
Rais wa Kongo Felix Tshisekedi anatafuta kuungwa mkono huku vita vikiendelea mashariki, lakini hadi sasa amerejea mikono mitupu kutoka katika ziara zake nje ya nchi huku wasiwasi ukiongezeka nchini mwake.
Imechapishwa:
Dakika 3
Matangazo ya kibiashara
Tshisekedi alizuru Angola hivi majuzi na kuhudhuria mkutano wa usalama mjini Munich bila kuleta mafanikio yoyote ya kidiplomasia, baada ya wapiganaji wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kudhibiti miji miwili mikubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hii inafuatia kushindwa kwa jeshi la Kongo, FARDC, dhidi ya M23 katika eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa DRC, ambalo limesambaratishwa kwa zaidi ya miongo mitatu kutokana na vita na mapigano kati ya makundi hasimu yenye silaha.
Kwa usaidizi kutoka kwa Rwanda – pamoja na kwamba Kigali inakanusha hilo – M23 wamelilemea jeshi la Kongo kwenye uwanja wa vita, jambo ambalo wachambuzi wanasema ni aibu ya kisiasa kwa rais wa DRC.
“Kutokuwa na uwezo wa kubadilisha nguvu za kijeshi kunazua swali la majukumu ya kiongozi mkuu wa jeshi (Tshisekedi),” amesema Trésor Kibangula, mchambuzi wa masuala ya siasa katika taasisi ya utafiti ya Ebuteli huko Kinshasa, mji mkuu wa DRC.
“Changamoto kwa rais sasa ni kuzuia mzozo huu kuwa kidokezo ambacho kinatishia uthabiti wa mamlaka yake,” ameongeza.
Kulingana na chanzo kilicho karibu na ofisi ya urais, kuna wasi wasi ndani ya baraza la mawaziri la Tshisekedi, ambapo “hali ya kumalizika kwa utawala” inatawala.
Mjini Kinshasa, mji mkuu wa DRC, wafanyakazi wengi wa mashirika ya kimataifa tayari wameondoka nchini kwa hofu ya nini kitatokea baadaye.
Washirika wa karibu wa Tshisekedi wamerudia katika siku za hivi karibuni kwamba “alichaguliwa kwa miaka mitano” na kuonya dhidi ya “mapinduzi” au “kuvuruga taasisi.”
Katibu mkuu wa chama cha rais, UDPS (Muungano wa Demokrasia na Maendeleo ya Kijamii), ametangaza kuwa “Félix Tshisekedi hatajiuzulu kamwe.”
Tshisekedi alichaguliwa mwezi Desemba 2023 kwa muhula wa pili kwa zaidi ya 70% ya kura rasmi.
Muungano wa vyama vinavyomuunga mkono pia una wabunge wengi katika Bunge la taifa.
Lakini alipoingia mamlakani baada ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2018, tume ya uchaguzi iliripoti kasoro ambazo waangalizi wanasema zilidhoofisha uhalali wake tangu mwanzo.
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi wakati huo alikuwa Corneille Nangaa, kiongozi wa muungano wa makundi ya waasi likiwemo kundi la M23.
Rwanda inakanusha kuhusika kwa kijeshi moja kwa moja katika mzozo huo, lakini wataalam wa Umoja wa Mataifa walisema mwaka jana kuwa nchi hiyo ilikuwa na wanajeshi 4,000 wanaofanya kazi pamoja na M23 na wanadhibiti kundi hilo.
Hadi sasa, juhudi za Tshisekedi na jumuiya ya kimataifa kuomba vikwazo dhidi ya Rwanda kwa uungaji mkono wake wa M23 hazijafanikiwa.
Alisafiri hadi Luanda siku ya Jumanne kukutana na Rais wa Angola Joao Lourenço, ambaye ameongoza juhudi za upatanishi za Umoja wa Afrika kusuluhisha mgogoro wa mashariki mwa nchi hiyo.
Waawili hao walizungumza wakati wa “mkutano wa kidiplomasia katika mazingira ya matukio ya hivi majuzi,” ambayo yanaibua “suala la hatua zinazopaswa kuchukuliwa”, kulingana na Angola.
Pia alimshutumu mtangulizi wake na sasa mpinzani Joseph Kabila – ambaye anasemekana kuondoka DRC tangu kuondoka madarakani – kwa kushirikiana na Rwanda kuchochea “mapinduzi haya dhidi ya jamhuri”.
Si Umoja wa Mataifa wala Umoja wa Ulaya ambao wameitikia wito wa DRC wa kuiwekea vikwazo Kigali.
Rais wa Rwanda Paul Kagame tayari amesema kwenye vyombo vya habari kwamba “hakuna mtu atakayemtisha kwa vitisho vya kuwekewa vikwazo.”
Ingawa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza imemwita mwanadiplomasia mkuu wa Rwanda mjini London, kuna dalili chache za wazi kwamba Tshisekedi anaungwa mkono katika juhudi zake za kuanzisha vita vya kidiplomasia dhidi ya Kigali.
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika sasa wanahofia kwamba mzozo huo unaweza kushika kasi na kuwa vita vya kikanda.
Paul-Simon Handy, mkurugenzi wa kanda ya Afrika Mashariki katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama (ISS), anasema kuwa “kuimarisha taifa la Kongo” na “taifa lenye uwezo wa kulinda mipaka yake” ni muhimu ili kuhakikisha utulivu katika eneo la Maziwa Makuu.