Vita kuendelea leo Europa League

Vita ya kuwania nafasi ya kuwamo kwenye nane bora ya mikikimikiki ya Europa League kinaendelea usiku wa Alhamisi, ambapo nyasi za viwanja vinane tofauti zitawaka moto kusaka timu zitakazoingia katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Athletic Bilbao baada ya kuchapwa 2-1 ugenini huko Italia mbele ya AS Roma, itakuwa nyumbani San Mames kujaribu kupindua matokeo hayo kusaka tiketi ya robo fainali, kama ilivyo kwa Ajax, ambayo ilikubali kuchapwa 2-1 nyumbani kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Eintracht Frankfurt, itakuwa ugenini kujaribu kupindua meza.

Lazio baada ya kushinda 2-1 kwenye mechi ya kwanza ilipocheza ugenini, itashuka uwanjani kwao kuikaribisha Viktoria Plzen katika moja ya mechi zinazotazamiwa kuwa na upinzani mkali ndani ya uwanja, huku kasheshe jingine litakuwa huko Ugiriki, wakati Olympiacos itakapojaribu kupindua matokeo ya kipigo cha mabao 3-0 ilichokipata kwenye mechi ya kwanza itakapoikaribisha Bodo/Glimt. Mashabiki wengi wanasubiria mechi hiyo kuona maajabu ya mpira yanavyoweza kufanyika kwenye mikikimikiki hiyo ya Europa League.

Lyon ilipata ushindi safi kabisa wa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza dhidi ya FCSB ilipocheza ugenini, hivyo usiku wa Alhamisi itakuwa nyumbani kumalizana na wapinzani wao hao, ambao watahitaji kufanya muujiza kwenye uwanja wa ugenini ili kutinga hatua inayofuata.

Balaa zaidi litakuwa huko Old Trafford, wakati Manchester United itakapokipiga na Real Sociedad katika mechi kali kabisa, ambayo itakuwa kama vile inaanza baada ya mchezo wao wa kwanza uliofanyika San Sebastian kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Man United inaitazama michuano ya Europa League kama tiketi ya kurudi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, hivyo inahitaji ushindi wa kutinga robo fainali kuzidi wapinzani wao, jambo litakalofanya mechi hiyo kuwa na upinzani mkali zaidi.

Jose Mourinho na kikosi chake cha Fenerbahce anaamini anaweza kwenda kupindua meza ugenini baada ya kikosi chake kukumbana na kipigo cha mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza ilipomenyana na Ranges huko Istanbul. Na sasa, Fenerbahce inakwenda Scotland kujaribu kupata ushindi utakaoweza kuwafanya wapenye na kutinga robo fainali ya michuano hiyo. Wataweza?

Kipute kingine kitakuwa huko London, wakati Tottenham Hotspur itakapokuwa nyumbani kuikaribisha AZ Alkmaar huku ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa bao 1-0 kwenye mechi ya kwanza waliyocheza ugenini. Spurs inahitaji ushindi ili kusonga hatua inayofuata, lakini inakumbana na AZ, ambayo ina rekodi ya kushinda mara nane kati ya mechi tiza za michuano ya Uefa inayohusisha mechi za nyumbani na ugenini. Spurs itatoboa? Kazi ipo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *