Vita dhidi ya utumikishwaji watoto hawa imetushinda?

Miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na ongezeko kubwa la utumikishwaji wa watoto, hasa wenye umri kuanzia miaka 12 hadi 15, katika biashara ndogondogo maeneo mengi nchini.

Watoto hawa utawaona wakiwa barabarani au vijiweni wakiuza bidhaa mayai maji, karanga, ubuyu nyinginezo.

Aidha, wapo wanaofanya biashara zao kwa kutembeza kwenye kumbi za starehe na mikusanyiko ya watu.

Utumikishwaji wa watoto katika biashara si tatizo jipya, linajitokeza katika maeneo mengi duniani, na hapa nchini limekuwa sugu na linaendelea kuwa changamoto kubwa kwa jamii.

Watoto hawa hufanya kazi kwa muda mrefu juani huku wakilipwa ujira mdogo na wengine kutolipwa kabisa, hivyo kupata madhara ya kiafya na kisaikolojia.

Madhara ya utumikishwaji huu ni pamoja na kupoteza fursa za elimu, athari za kiafya kutokana na kufanya kazi kwenye mazingira magumu.

Katika hali hii watoto hawa wanakuwa na uwezo mdogo wa kujijenga na kujiandaa kwa maisha yao ya baadaye, jambo ambalo ni hatari si kwao tu bali hata kwa nchi.

 Uzoefu unaonyesha familia nyingi hapa nchini zina changamoto kubwa ya kifedha, matokeo yake watoto wanashirikishwa katika biashara kama njia ya kuongeza kipato cha familia.

Ni ama wazazi wao ndio wanaowatuma kufanya biashara, au wenyewe wanaamua kujitosa huko kutokana na mazingira magumu ya kimaisha katika familia zao.

Sababu nyingine ya kukithiri tatizo la utumikishwaji watoto, ni walezi wengi kukosa uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto wao.

Pia maeneo mengi ya nchi, miongozo ya Serikali inayohusu kulinda haki na vita dhidi ya utumikishwaji wa watoto, haitekelezwi ipasavyo.

Hiyo ni kwa sababu hakuna mikakati madhubuti ya kuwabana wazazi na walezi wanaowatumikisha watoto kwenye shughuli hizi.

Tatizo la utumikishwaji watoto limekuwa likiathiri mataifa mbalimbali duniani na baadhi yao, zimeweza kukabiliana nalo kwa kutumia mbinu sahihi na hatimaye kulimaliza.

 Katika miji ya India kwa mfano, utumikishwaji wa watoto katika biashara ndogondogo kama kuuza mayai maji ulizidi kuwa tatizo miaka ya nyuma.

Hata hivyo, serikali ilianzisha kampeni kubwa ya elimu kwa jamii na sheria kali dhidi ya wafanyabiashara wanaowatumia watoto kufanya biashara.

Baadhi ya njia zilizotumika na taifa hilo ni kulenga familia kwa kutoa misaada ya kifedha na program za elimu, ili kuzuia watoto kujihusisha na biashara za mitaani.

Hata majirani zetu wa Kenya nao walishawahi kukumbwa na changamoto hiyo ya utumikishwaji wa watoto katika miji kama Nairobi na mingineyo.

 Katika kukabiliana na hali hiyo, serikali na mashirika ya kiraia zilijikita katika kutoa elimu na kusaidia watoto waliokuwa wakifanya biashara za mitaani kwa njia ya kuwapatia mafunzo ya ufundi na kuwasaidia kurudi shule.

Mkalati huo uliwezesha kupunguza idadi ya watoto wanaojihusisha na biashara hizo.

Si vibaya kujifunza kwa waliofanikiwaa. Tunaweza kutumia njia zilizotumiwa na wenzetu au nyinginezo, alimradi tu zinatoa hamasa kwa wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto wao.

 Serikali na mashirika binafsi yanapaswa kutoa elimu kuhusu madhara ya kumtumikisha mtoto na faida za kumwacha mtoto apate elimu.

Misaada ya kifedha pia inaweza kutolewa kwa familia maskini ili kupunguza utegemezi wa watoto kama chanzo cha mapato.

Mbali na hilo njia nyingine ni Serikali kuongeza makali juu ya sheria za kulinda haki za watoto, ili ziiimarishwe na kutekelezwa kwa ukamilifu.

Hii inajumuisha kutoa adhabu kali kwa wazazi au walezi, wanaowatumia watoto kwa shughuli za kibiashara.

Njia nyingine ni Serikali kuweka mifumo ya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya miji, ili kuhakikisha kwamba watoto hawatumikishwi kwa namna yoyote ile.

Tuanzishe vituo vya mafunzo kwa watoto, ili kuwapa fursa ya kujifunza ujuzi wa mbalimbali badala ya kujihusisha na biashara za mitaani.

Aidha, ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, mashirika binafsi na jamii, ni muhimu katika kudhibiti na kukomesha utumikishwaji wa watoto.

Bila ya juhudi na mikakati ya pamoja kama Watanzania, sioni kama tunaweza kuishinda vita hii inayowakosesha watoto haki zao za kimsingi za kibinadamu.

Ni muhimu kuchukua hatua za haraka ili kulinda haki za watoto, kuwapa elimu bora, na kuwawezesha kujijenga kwa mustakabali wa maisha yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *