Viongozi wanawake wapeana mbinu kuwainua wenzao

Arusha. Wanawake wenye nafasi katika maeneo ya uhifadhi, utafiti na usimamizi wa rasilimali za asili nchini, wametakiwa kuondoa hofu na kuvunja vikwazo kwa kuongeza juhudi ili kuhakikisha vizazi vijavyo vinarithishwa Tanzania endelevu.

Pia, imeelezwa kuwa, uwekezaji kwa wanawake katika sekta ya utalii kupitia nyanja mbalimbali ikiwamo ya utafiti na uhifadhi ni uwekezaji hai kwa mazingira ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Hayo yamesemwa jana Jumamosi Machi mosi, 2025 na Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) Kanda ya Kaskazini, Steria Ndaga alipozungumza na wanawake watumishi kutoka hifadhi tano za Taifa zilizopo kanda ya kaskazini waliotembelea Hifadhi ya Ziwa Manyara kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani.

Ndaga  amesema: “Sisi ndiyo mabalozi wa kwanza wa utalii unaotokana na juhudi zetu za kulinda na kuhifadhi maeneo haya. Tuendelee kujenga mazingira yanayowezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika uhifadhi na maendeleo, tutaongeza kasi ya maendeleo na kuhakikisha maliasili zetu zinalindwa kwa manufaa ya sasa na baadaye.

“Nawahimiza tuendelee kujenga fursa za kufanya kazi pamoja, tuwavute na ambao wako nyuma lengo kina mama tusonge mbele, tumepewa nafasi za uongozi katika hifadhi na taasisi mbalimbali, tuzitumie hizi nafasi vizuri na tuwe mfano, tusiwe na hofu katika utekelezaji wa majukumu yetu.”

Ndaga amesema ziara hiyo ni sehemu ya wiki ya wanawake kabla ya kufikia kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake.

Amesema watumishi hao zaidi ya 150 wametoka katika hifadhi za Tarangire, Ziwa Manyara, Mkomazi, Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro na wengine kutoka Tanapa makao makuu.

Mkuu wa hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dk Yustina Kiwango amesema katika maadhimisho ya mwaka huu mbali na kuhamasisha utalii wa ndani, wanawake hao watatembelea na kutoa misaada kwa makundi maalumu ili kuzidi kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Amesema kutokana na sekta ya utalii pekee kuliingizia Taifa asilimia 21 ya fedha za kigeni, wataendelea kutumia nafasi zao kuchangia uchumi wa nchi kwa kulinda uhifadhi na rasilimali za asili kwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kila mmoja kutimiza wajibu wake.

Mmoja wa wanawake hao, Upendo Ngowo amesema ni muhimu elimu na uhamasishaji wa wananchi kutembelea hifadhi za Taifa nchini zinapaswa kutolewa hasa kwa jamii za pembezoni.

“Kiukweli jambo hilo ni muhimu na zuri, wadau wakiungana kwa pamoja kutoa elimu na kuhamasisha jamii hasa za pembezoni itasaidia kuongeza watalii wa ndani na kukuza pato letu,” amesema.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, kitaifa yatafanyika Machi 8, 2025 mkoani Arusha huku mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kabla ya kilele cha maadhimisho hayo shughuli mbalimbali zinatarajiwa kufanyika ikiwamo michezo ya timu za wanawake, usiku wa mwanamke, nyama choma na wanawake katika makundi mbalimbali kutembelea vivutio vya utalii.

Shughuli nyingine ni elimu na msaada wa kisheria, utatuzi wa migogoro ya ardhi na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kutoa kipimo maalumu cha uchunguzi wa moyo wa mtoto aliye tumboni.