
Katika jamii yoyote yenye maendeleo, viongozi wa umma wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanawahudumia wananchi kwa uadilifu, heshima na weledi.
Moja ya mambo yanayochangia maendeleo ni mawasiliano mazuri kati ya viongozi na wananchi.
Kwa kuzingatia hilo, Februari 3, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan aliweka msisitizo wa suala la maadili ya viongozi alipokuwa akizungumza na majaji wakati wa maadhimisho wa Siku ya Sheria nchini, yaliyofanyika jijini Dodoma.
Rais Samia hakumung’unya maneno, aliwataka viongozi wa mhimili huo wa mahakama wasijigeuze miungu watu kwa nafasi waliyokuwa nayo, bali watende haki, wasichukue nafasi ya Mungu.
Desemba 17, 2024 Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Simbachawene alizitaka mamlaka za nidhamu kuchukua hatua stahiki na kwa wakati kwa watumishi wanaokwenda kinyume na maadili yao ya kazi, akijikita zaidi kuelezea tabia ya kughushi barua za uhamisho, huku akiwasisitiza katika zama hizi mambo yanavyosambaa kwa haraka watu wafanye kazi kwa weledi.
Mifano hiyo, inatukumbusha tukio lililotokea mkoani Tabora usiku wa kuamkia juzi, ambapo Meneja wa Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA) mkoani humo alijikuta matatani akidaiwa kumtolea lugha isiyofaa Mkuu wa Mkoa, Paul Chacha na watumishi wengine wanane kutoka ofisi ya Waziri Mkuu kwa kile kinachoelezwa kuwa alikuwa amelewa alipofanya hivyo.
Hiyo ni taswira ya jumla, lakini huko katika ofisi za umma kumekuwa na changamoto kubwa ambapo baadhi ya viongozi wanatumia kauli zisizofaa wanapowasiliana na wananchi, hali inayosababisha migogoro, kutoelewana na hata kupunguza imani ya wananchi kwa Serikali.
Ni muhimu kwa viongozi wa umma kujiepusha na lugha zisizofaa na badala yake kuzingatia sheria ya maadili ya utumishi wa umma, ili kuhakikisha huduma bora kwa wananchi. Kauli zinazotolewa na viongozi zinaweza kuwa na athari chanya au hasi katika jamii. Matumizi ya lugha yenye heshima yanasaidia kujenga mazingira ya kuheshimiana kati ya viongozi na wananchi. Viongozi wa umma wanapaswa kutumia lugha inayozingatia heshima, upendo, na mshikamano ili kuepusha migawanyiko katika jamii.
Katika mazingira ya kidemokrasia, wananchi wanahitaji kusikilizwa kwa makini na viongozi wanapaswa kutumia lugha inayohamasisha suluhisho badala ya kuibua migogoro.
Maneno ya dharau, kejeli au vitisho yanawafanya wananchi kupoteza imani kwa Serikali na kuathiri ufanisi wa utoaji wa huduma za umma.
Katika nchi nyingi, sheria za maadili kwa watumishi wa umma zimewekwa ili kuhakikisha viongozi wanafanya kazi zao kwa uwajibikaji na heshima.
Sheria hizi zinawataka viongozi wa umma kuwa waadilifu, wenye heshima na wanaotanguliza masilahi ya wananchi mbele ya masilahi binafsi.
Kwa mfano, katika Tanzania, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inawataka viongozi kuwa na nidhamu katika mawasiliano na kuepuka lugha au matamshi ambayo yanaweza kudhalilisha wananchi. Kiongozi wa umma anapaswa kuwa kielelezo kwa jamii kwa kuonyesha mfano mzuri.
Kuhudumia wananchi inahitaji weledi mkubwa kutoka kwa viongozi wa umma. Weledi unahusisha kuwa na ujuzi wa kazi, uadilifu na kujituma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Viongozi wa umma wanapaswa kuelewa kuwa wao ni watumishi wa wananchi na si waajiri wao, kwa sababu kodi za wananchi ndizo zinawalipa mishahara na marupurupu ya kila aina. Sheria za maadili zinapaswa kutekelezwa kikamilifu ili kuhakikisha viongozi wanatumia lugha nzuri kwa wananchi.