
Wakuu wa nchi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC watakutana tena wiki ijayo, kujadili hali inavyoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Rais wa Kenya William Ruto, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ametangaza hili kupitia ukurasa wake wa kijamii wa X, baada ya kukutana na mwenzake wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, Mwenyekiti wa SADC walipokutana jijini Windhoek nchini Namibia, siku ya Ijumaa.
Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika kwa njia ya video, baada ya viongozi wa jumuiya hizo mbili kukutana jijini Dar es salaam, nchini Tanzania mwezi Februari, ambako walitoa wito wa usitishwaji vita na kutaka mazungumzo kutumiwa kupata suluhu.
Licha ya wito huo, waasi wa M23 wameendelea kusonga mbele na kuchukua maeneo kadhaa, wiki hii wakiuteka mji wa Walikale, baada ya kuteka miji mikubwa ya Goma na Bukavu.
Wiki hii mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali ya Kinshasa, na waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda, yalitarajiwa kuanza jijini Luanda nchini Angola, lakini hayakufanyika baada ya M23 wanaosema wako tayari kwa mazungumzo kuyasusia, wakilalamikia hatua ya Umoja wa Ulaya kuwawekea vikwazo baadhi ya viongozi wake.
Siku ya Jumanne, rais Felix Thisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame, walikutana jijini Doha baada ya mwaliko wa nchini Qatar, katika kikao ambacho hakikutarajiwa, huku viongozi hao wakikubaliana usitishwaji wa vita Mashariki mwa DRC.