Viongozi wa Kiislamu na wa Kiarabu ambao wameitisha mkutano wa dharura mjini Riyadh Saudi Arabia wameutaka utawala wa Kizayuni ukomeshe mara moja jinai zake za kinyama katika Ukanda wa Ghaza na Lebanon.
Miongoni mwa viongozi hao ni Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, Mohammad bin Salman ambaye katika hotuba yake kwenye mkutano huo wa dharura wa pamoja wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) jana Jumatatu, alilaani mauaji yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina na Lebanon na kuutaka utawala wa Kizayuni “kujiepusha na kitendo chochote cha uchokozi.” Bin Salman amelaani pia mashambulizi ya Israel nchini Iran.
Kwa upande wake, Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, naye amejiunga na mwanamfalme wa Saudia kulaani jinai za kinyama na uharibifu mkubwa unaofanywa na Israel huko Ghaza na Lebanon. Amesema: “Maneno hayawezi kuelezea hali mbaya ya wananchi wa Palestina.”

Akihutubia katika mkutano huo, Rais Mahmoud Abbas wa Palestina amezitaka nchi za Kiarabu na Kiislamu kushikamana vilivyo na wananchi wa Palestina.
Pia ametaka kutekelezwa azimio la Umoja wa Mataifa la kukomesha jinai za Israel huko Ghaza na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inafikishwa katika eneo hilo.
Zaidi ya viongozi 50 wa nchi za Kiarabu na Kiislamu wameshiriki kwenye mkutano huo wa dharura wa mjini Riyadh.
Kabla ya mkutano huo, Hamas ilitoa mwito wa kuundwa muungano wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu ili kuishinikiza Israel na waitifaki wake wakomeshe ukatili wao Ghaza na Lebanon.