Viongozi wa dini watoa ujumbe wa Idd

Dar es Salaam. Katika kuadhimisha Sikukuu ya Idd El-Fitr, viongozi wa dini ya Kiislamu nchini wameshauri Watanzania kutotumika kuvuruga amani ya nchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.Mbali na kulinda amani, viongozi hao wamesisitiza wananchi kushiriki siasa safi na kila mwenye uwezo wa kugombea nafasi za kisiasa kwenye uchaguzi huo wa madiwani, wabunge na urais kujitokeza kuomba ridhaa hiyo.Msisitizo mwingine uliowekwa na viongozi hao ni wao wenyewe kuwa mfano bora wa mapatano kwenye jamii na kuepuka chuki, huku wakihimiza wananchi kuendelea kutenda mema kama ilivyokuwa wakati wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.Kauli hizo zimetolewa leo, Jumatatu, Machi 31, 2025, kwa nyakati tofauti na viongozi wa dini ya Kiislamu katika swala ya Idd El-Fitr iliyofanyika maeneo mbalimbali nchini.Swala ya Idd kitaifa imefanyika katika Msikiti wa Mfalme Mohammed VI wa Morocco, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, na viongozi mbalimbali wameshiriki, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.Kuhusu uchaguzi mkuu, Imamu wa Masjid Rahma, uliopo Kata ya Lukobe, Manispaa ya Morogoro, Sheikh Faraji Jongo, amewataka Watanzania kutotumika kuchafua amani ya nchi kwa kutoa kauli zenye uchochezi na kashfa kwa viongozi wakuu wa nchi.”Amani tuliyonayo inatufanya sisi Waislamu tusali kwa amani, na hata wenzetu wasiokuwa Waislamu nao kufanya ibada kwa amani. Zipo nchi leo hii yawezekana wanaswali Idd huku wamesimamiwa na watu wenye mitutu ya bunduki. Tuilinde tunu hii ya amani kwa kuwa ikitoweka, hakuna atakayekuwa salama,” amesema.Kauli hiyo haitofautiani na iliyotolewa na Sheikh wa Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, Ramia Isanga, akisisitiza Waislamu kuyaendeleza mema waliyokuwa wakiyafanya kipindi cha mwezi mtukufu ili kuachana na dhambi na kuepuka vurugu wakati wa uchaguzi.”Tunatarajia mambo mema yataendelea kufanyika; uhuni, wizi, zinaa, ulevi na mambo mengine machafu hatutegemei kuyaona, zaidi ya kuswali na kumrudia Mungu,” amesema Sheikh Isanga.Pia, ameitaka jamii kuombea Uchaguzi Mkuu 2025 ili uwe wa amani na kuhakikisha wanachagua viongozi bora.Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke, amewatahadharisha Watanzania kutokubali kuingia mtego wa kujiingiza kwenye maandamano ya kisiasa yanayoweza kuhatarisha amani ya nchi.”Watanzania, tuienzi amani. Waislamu, dini yenu ni ya amani, unyenyekevu, ndiyo maana ikaitwa Al-Islam. Ukikutana na mtu akaanza kukupigia maneno bila kukuhakikishia amani, usimjibu. Mwambie tu ‘Assalam Alykum’ (Amani iwe juu yako),” amesema Sheikh Kabeke na kuongeza:”Waislamu, hata wasiokuwa Waislamu, chukueni fomu bila kuangalia chama unachogombea. Asibakie Muislamu akisema kwamba suala la uchaguzi siyo letu. Sisi ni raia wa nchi hii, tuna haki ya kugombea, kuchagua na kuchaguliwa. Nendeni mkachukue fomu,” amesisitiza.Kauli hiyo inaungwa mkono na Imamu wa Msikiti wa Muuminina, Kibaha Mailimoja, Mkoa wa Pwani, Yusuph Masood, akisema ni muhimu Watanzania kujitokeza kugombea nafasi za uongozi ili kuwa na mchango wa maendeleo nchini. Alichokisema MuftiKatika maelezo yake aliyoyatoa kwenye swala ya Idd, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir, amewataka viongozi wa dini ya Kiislamu kuwa mfano bora wa mapatano kwenye jamii.”Hii ni siku ya kushikamana sana na ni siku ya kuondosha vifundo. Wale waliogombana leo wapatane, kwa sababu ukifanya hivyo utaingia peponi na milango itafunguka. Mungu hatufundishi tusipatane. Ugonjwa huu ni mbaya sana na upo kwa masheikh; wengine hawakubaliani, mwingine anajua kuliko mwingine. Pataneni masheikh, nataka muonyeshe mfano,” amesisitiza Mufti.Sheikh Abdallah Al Mundhir wa Msikiti wa Mtoro, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, amehimiza Watanzania kuendeleza mema kwa kuwa jambo hilo ndilo analotaka Mungu.”Saidieni wasiokuwa na uwezo, muwape wale ambao hawana. Endelezeni yale mliyoyafanya wakati wa Ramadhani. Kama uliweza kujizuia kuyafanya wakati huo, kwa nini usiweze wakati wa miezi ya kawaida?” amesema Sheikh Mundhir.Katika kushughulikia suala la maadili, Sheikh wa Msikiti wa Rahman, uliopo Buhongwa, jijini Mwanza, Ibrahim Suleyman, amesisitiza Watanzania kuendeleza mema waliyotenda mwezi wa Ramadhani.”Tumuombe Allah atujalie kwamba mwezi wa Ramadhani huu uliopita uwe sababu ya watu kuacha maovu, kupendana na kuishi kama Allah alivyotwambia. Mcha Mungu huwa anasamehewa makosa yake,” amesema Sheikh Suleyman.Amesisitiza kuwa Tanzania inahitaji amani na ili kuidumisha, ni vyema kutenda yaliyo mema kwenye jamii na kuzingatia utu.Hoja hiyo ni sawa na iliyosemwa na Sheikh wa Wilaya ya Shinyanga, Soud Kategile, ambaye amesisitiza kutenda mema na kuchagua viongozi bora.“Nawasihi, ni vyema mkiendelea kuishi kwa kutenda mambo yaliyo mema, kufuatilia na kusoma mafundisho ya Mungu. Kuweni makini kuchagua viongozi wanaopenda maendeleo ya watu na siyo watoa pesa. Wanaotanguliza pesa hawajali maslahi ya wananchi,” amesema.Naye Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Ayas Njalamba, alihitimisha swala ya Idd akiwataka vijana wasiengeuke kimaadili.“Tumejikita kuwapeleka watoto wetu katika shule za elimu ya kimazingira na kusahau elimu ya dini. Vijana wanajibadili tofauti na walivyoumbwa, na kusababisha matendo yasiyo na maadili,” amesema. Imeandikwa na Saddam Sadick (Mbeya), Hellen Mdinda (Shinyanga), Hamida Shariff (Morogoro), Saada Amir (Mwanza), Joseph.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *