
Dar es Salaam. Viongozi wa dini nchini wamehimizwa kusema ukweli kuhusu mambo yanayotokea katika jamii kwa kuwa wao wanaaminiwa na Watanzania, hivyo wasiogope kutishwa.
Hayo yamebainishwa na wadau mbalimbali kwenye mkutano wa Jukwaa la Dini Mbalimbali uliofanyika jana Novemba 7, 2024 jijini Dar es Salaam ukiwakutanisha viongozi wa dini, wanazuoni na asasi za kiraia.
Jukwaa na Dini Mbalimbali limeanzishwa likilenga kuwakutanisha viongozi wa dini kujadili mambo yao likihusisha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Mkutano huo ulijadili masuala ya kitaifa yanayohusu dini, maendeleo, siasa na maadili; msisitizo ukiwa ni kwa viongozi wa dini kusimamia ukweli na kuwahimiza waumini kuwa wa kweli.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa TEC, Padri Charles Kitima amesema kauli za kwamba viongozi wa dini wanaingilia siasa zinatumika kuwarudisha nyuma ili wasitende haki au kuzungumzia mambo yanayotokea kwenye jamii.
“Viongozi wa dini tunafundisha watu kusimamia ukweli kwa gharama yoyote, kwa hiyo tusiogope kutishwa,” amesema.
Padri Kitima ambaye ni mmoja wa viongozi wa jukwaa hilo, amesema Watanzania wanajua viongozi wa dini ndio kimbilio mbadala pale wanapoona wamekwama na wanahitaji mtu wa kuwasemea ili changamoto zao zitatuliwe.
Amesisitiza asasi za kiraia zinahitaji kujengewa uwezo zitekeleze majukumu yao ipasavyo hasa kutoa elimu ya uraia kwa wananchi.
“Tunahitaji kushirikiana katika kuwasaidia wananchi, viongozi wa dini tutimize wajibu wetu ipasavyo na asasi za kiraia nazo zifanye kazi kwa bidii kuwasaidia Watanzania,” amesema.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh amesema ni muhimu siasa za Tanzania zikafanyika katika kweli, badala ya chuki ambazo zinahatarisha amani.
Ametoa mfano matokeo ya uchaguzi wa Marekani yaliyotolewa Novemba 6, 2024 ambayo mgombea wa Republican, Donald Trump alishinda uchaguzi huo na mpinzani wake, Kamala Harris akampigia simu kumpongeza kwa ushindi huo.
“Tuwe na huo moyo kama Marekani, Kamala ameshindwa kwenye uchaguzi, amempigia simu mwenziwe kumpongeza na sasa Marekani inaendelea mbele,” amesema.
Mhadhiri mstaafu, Dk Azaveri Lwaitama amewataka viongozi wa dini kusukuma ajenda ya kuwa na Katiba mpya kwa sababu kukosekana kwake ndiko kunasababisha matatizo sugu katika jamii.
Amewataka waandae kijitabu kidogo ambacho kitaelimisha wananchi kuhusu Katiba mpya na kuwafanya kuwa sehemu ya mchakato huo ambao unakwamishwa na wanasiasa kwa masilahi yao ya kisiasa.
“Tunahitaji Katiba mpya kwa sababu madaraka ya nchi hii yamehodhiwa na kikundi kidogo cha watu, jambo ambalo linadhoofisha maendeleo ya wengine. Kwa hiyo, hata mfumo wa maisha umedhoofishwa.
“Jukwaa la Interfaith (Dini Mbalimbali) lisimamie jambo hili ili angalau tupate rasimu ya mwisho itakayobeba maoni ya wananchi. Tuchukue vitu kwenye rasimu ya Jaji Warioba, na vingine kwenye Tume ya Jaji Nyalali na Jaji Kisanga,” amesema.
Katibu Mkuu wa Bakwata, Nuhu Mruma amesema Jukwaa hilo linasaidia kuondoa makando-kando yanayojitokeza katika jamii ili kuleta usawa na kuwafanya Watanzania waishi kwa amani na umoja licha ya tofauti zao.
Amesema viongozi wa dini wanafanya kazi ya kuondoa changamoto zinazojitokeza katika jamii ili kuleta usawa.