
Dar/mikoani. Viongozi wa dini ya Kiislamu nchini, wamesisitiza uzingatiaji wa demokrasia ikiwamo kukaa mezani kujadili kwa pamoja wanapohisi kuna kutoelewana.
Viongozi hao wametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti ikiwa ni katika kusherehekea Idd El Fitr ikiwa ni kuhitimisha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Katika nasaha za viongozi hao wamesisitiza mambo manne yazingatiwe nchini ikiwemo viongozi wa kisiasa kukaa meza ya mazungumzo kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 2025.
Mambo mengine yaliyosisitizwa na viongozi hao ni kuendelea kuisimamiwa haki na demokrasia na kuepuka rushwa na kuwapata viongozi watakaowawakilisha wananchi na kuendeleza maadili mema yaliyokuwa yakifanyika kwenye mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani,
Katibu Mkuu wa Shura ya Maimam, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema vyama vya siasa vimetoa msimamo mzito hasa kuzuia uchaguzi akisisitiza upo umuhimu wa viongozi serikalini kukutana na kurekebisha hali iliyopo.
“Tumeona baadhi ya vyama vya siasa vimetoa tamko zito na misingi wanayosimamia, mfano wamesema watazuia uchaguzi kwa sababu kuna wanayotaka yarekebishwe, ipo haja ya viongozi kukutana kuangalia hali hiyo ikoje, hili si jambo la kupuuzwa hata kidogo nchi isije kuingia kwenye matatizo,” amesema.
Sheikh Ponda amesema ni muhimu kuchukuliwa hatua za haraka za kuzuia tatizo na si kulisubiri kulitibu.
Hoja ya uchaguzi imezungumzwa pia na Shekh Hilal Shaweji, maarufu Shekh Kipozeo amesisitiza ni muhimu viongozi kutambua changamoto inapojitokeza ndani ya nchi, badala ya kusubiri iwe ugonjwa wa kuja kuutibu.
“Watu lazima waelewa balaa linapotokea linakuwa balaa kwelikweli, ni bora zaidi kuchukua hatua za kuzuia kuliko kutibu,” amesema.
Wakati, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania TIC Maulana, Sheikh Hemedi Jalala Mwakindenge amesisitiza viongozi wa kisiasa na Serikali kuzingatia haki na demokrasia kwenye uchaguzi mkuu.
Amesema suala la amani ndilo linalofanya Watanzania kumwabudu Mungu na kuendelea na shughuli za uzalishaji mali, akibainisha amani ikitoweka hakuna litakalofanyika nchini.
“Demokrasia na haki zifunikwe na mwamvuli wa amani na mshikamano, Watanzania wanaona, amani tuliyonayo ni neema kubwa tuliyopewa na Mungu kwa hiyo si sawa kuifanyia mchezo, kuichezea au kuifanya amani tuliyonayo ikaathirika,” amesema.
Sheikh Jalala amesema kwa yeyote anayedai haki yake ya kisiasa aitafute kwa amani kwani haitakuwa vyema kudai haki kwa kuvunja amani.
Hoja hiyo ya uchaguzi inaendelezwa na Sheikh wa Mkoa wa Manyara, Mohamed Kadidi amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi huku akikemea vitendo vya rushwa.
Amesema ni muhimu maadili yakazingatiwa ikiwemo kutokujihusisha na vitendo vya rushwa ili kuchagua viongozi watakaoharakisha maendeleo.
“Wito wangu kwa Waislamu na Watanzania kwa ujumla tuendelee kuwa watulivu tukitafakari uchaguzi mkuu wa mwaka huu tujitokeze kupiga kura kuchagua viongozi wanaofaa, tufanye uamuzi sahihi.”
“Tusijihusishe na vitendo vya kutoa au kupokea rushwa kwa sababu kura ni amana sasa unatakiwa uangalie amana yako unaitoa kwa nani ili akalete maendeleo kwa masilahi mapana ya Taifa,” amesema.
Katika msingi wa haki, Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Ayas Njalambaa amesema mwezi wa Ramadhani uwe sehemu ya kupitisha uchaguzi ulio bora, haki, amani na utulivu na akiomba kila mmoja kushiriki uchaguzi huo.
“Ramadhani hii iwe sehemu ya kutupitisha kwenye uchaguzi mkuu ambao utafanyika mwaka huu, kila mmoja ashiriki hatua hiyo kwa kutanguliza amani, utulivu na uzalendo ili tupate viongozi walio bora kutuongoza” amesema Sheikh Njalambaa.
Maadili na kuendeleza mema
Hata hivyo, kuhusu maadili ya jamii, Sheikh Jalala amesema lengo la mfungo ni kuwafanya watu kubadilika hivyo kila jema lililotendeka wakati wa mfungo anaamini yote yataendelezwa baada ya mfungo kutamatika.
Katika eneo la maadili, Sheikh Ponda amesema mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani huwajenga watu kuwa na mioyo ya huruma, kutii mambo bila shuruti ikiwemo kuepuka michezo ya kamari, uzinifu na unywaji wa pombe.
“Baada ya Ramadhani utatakiwa kuendelea kuyaishi mafundisho hayo, ni matarajio yetu baada ya mfungo kutakuwa na mabadiliko makubwa sana kwenye jamii na mabadiliko hayo yanapaswa kuanzia kwa viongozi,” alisema.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amewataka Waislamu na jamii kwa ujumla kuendeleza matendo na tabia njema walizokuwa wakifanya katika mwezi wa Ramadhani.
“Tuwe kama mfano wa gari iliyokwenda gereji na sasa iko safi, ni kama tulipelekwa katika ukarabati maalum wa tabia zetu hivyo miezi inayofuata tuendelee watu wema” amesema.
Vilevile amesisitiza jamii kuendelea kuishi kwa amani, umoja na ushirikiano.
Akizungumzia hilo, Qadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhan Kitogo amewataka Waislamu na Watanzania wote kuwa na maelewano na wenzao kama ilivyokuwa wakati wa mfungo.
“Tumekuwa na maadili mazuri mwezi wa Ramadhani, watu hawatukanani, hawasemi maneno ya hovyo, mienendo ilikuwa mizuri, maadili haya tuendelee nayo ili tuendelee kuwa watu wema,” amesema Sheikh Kitogo.
Alichokisema Mufti
Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuber Bin Ally amewataka Watanzania kuendelea kuyaishi yale yaliyofundishwa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kulinda amani na ndimi zao ili zisiwaumize wengine.
“Tunamaliza mwezi wa Ramadhani, nasaha zangu waliofunga na wasiofunga ni kuendelea kuyashika mafunzo yaliyotolewa ndani ya mwezi huo, tangazo letu la kwanza wakati tunaanza Ramadhani tulisema mwezi huu ni chuo kinachofundisha mambo mengi ikiwemo ucha Mungu hivyo tuliyoyapata mwezi huu tuyafanyie kazi,” amesema.
Mufti alitoa kauli hiyo jana usiku katika hafla ya chakula cha jioni (iftar) iliyoandaliwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC).
Kwenye hilo, Amira wa Baraza Kuu la Wanawake wa Kiislamu Tanzania, Fatma Mdidi amewasihi wazazi kuwa karibu na watoto kama mbinu mojawapo ya kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.
“Mmomonyoko wa maadili unaongezeka kutokana na wazazi kutotenga muda wa kukaa na watoto wao kuzungumza badala yake hutumia muda mwingi katika shughuli za kujitafutia riziki.
“Tutenge muda wa kukaa na watoto wetu ili kujua nini wanafanya kwa lengo la kupunguza kasi ya mmomonyoko wa maadili katika jamii”amesema.
Kuelekea uchaguzi mkuu, Fatma Mdidi amewataka wenye vigezo kujitokeza kupiga kura ili kutimiza haki yao ya kikatiba.
Vilevile aliwasihi kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoashiria kuvunja amani. Ya kuzingatia kabla, baada ya Sala ya Idd.
Pamoja na mambo mengine, Waislamu wamekumbushwa mambo ya kufanya kabla na baada ya kusali Idd.
Miongoni mwa waliyokumbushwa ni kubadili njia watakapokuwa wakirejea nyumbani baada ya sala ya Idd, huku sababu ikitajwa kuwa ni kutimiza Sunnah hiyo ya Mtume.
“Mtume Muhammad (S.A.W) kaelekeza hivyo, amesema njia utakayokwenda nayo ubadilishe upite nyingine baada ya sala ya Idd, unapofanya hivyo unapata thawabu kwa kufuata kile ambacho Mtume anataka,” amesema Sheikh Khamis Mataka ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata). Amesema ikitokea haujabadilisha njia haina shida, kwa sababu kikanuni kitu ambacho Mtume amekisema ukikitenda unapata thawabu, ila ukikiacha hupati dhambi.
“Usipokifanya hupati dhambi, lakini utakuwa umekosa fadhila na thawabu ukitoka kusali Idd,” amesema.
Mbali na kubadili njia, Sheikh Mataka amekumbusha kusema neno Takbir unapotoka nyumbani kwenda kusali Idd, akieleza hiyo ni ishara ya kumtukuza Mwenyezi Mungu.
“Hii ni sawa na kusema “Allahu Akbar, yaani Mwenyezi Mungu ni mkubwa.
Sheikh Mataka amesema jambo lingine ambalo waumini wa Kiislamu wanatakiwa kufanya baada ya kumaliza Ramadhan na kabla ya kuswali Idd ni kutoa Zakat ul-fitr.
“Zakat ul-fitr ni kutoa kiasi cha kilo mbili na nusu ya chakula kinachopendwa katika mji, hii inatakiwa itolewe kabla ya kusali, ukiitoa kabla ya kwenda msikitini kusali Idd, hapo ndipo inakuwa zakat ul-fitr.
“Ukiitoa baada ya kuswali hiyo itakuwa ni sadaka ya kawaida,” amesema.
Amesema katika swala ya Idd watu wanatakiwa wavae nguo nzuri, wakilimiane na kuendelea kufanya mema.
“Jambo kubwa zaidi ni watu kujiepusha na maasi na maovu kwa sababu Mtume Muhammad (S.A.W), kasema anayefanya maovu siku ya Idd ni kama anayemkosea Mwenyezi Mungu siku ya kiama,” amesema.
Imeandikwa na Baraka Loshilaa, Mariam Mbwana, Aurea Simtowe, Sute Kamwelwe, Imani Makongoro (Dar), Saddam Sadick (Mbeya), Janeth Mushi (Arusha).