Dar es Salaam. Viongozi wa Kampuni zilizo chini ya Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) wameapa kuendeleza maono ya Mtukufu Aga Khan IV katika taasisi wanazoziongoza ili kusaidia jamii na kuchochea maendeleo.
Viongozi hao wamebainisha hayo wakati wa ibada maalumu ya kumbukumbu ya Mtukufu Aga Khan IV, iliyofanyika leo Februari 7, 2025 jijini Dar es Salaam ikiwakutanisha pamoja viongozi na wafanyakazi wa kampuni hizo.

Mtukufu Aga Khan IV, Imamu wa 49 wa madhehebu ya Shia Ismailia, alifariki dunia Februari 4, 2025 jijini Lisbon, Ureno akiwa na umri wa miaka 88. Mwili wake unatarajiwa kuzikwa Jumapili Februari 9, 2025 mjini Answan nchini Misri.
Taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Imamu wa Shia Ismailia inaeleza kuwa, baada ya ibada maalumu ya mazishi itakayofanyika Jumamosi, jijini Lisbon, Ureno mwili wa kiongozi huyo utasafirishwa kwenda Misri kwa maziko.
Aga Khan IV ndiye mwasisi wa AKDN, mtandao unaofanya kazi ya kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, utamaduni na vyombo vya habari. Amewekeza katika nchi 30 duniani na kugusa maisha ya watu wengi.
Akizungumza kwenye ibada hiyo, Mjumbe wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Hanif Jaffer amesema kama chombo cha habari, watamkumbuka Aga Khan IV aliyeamini katika nguvu ya uhuru wa habari, kuchochea maendeleo katika nchi za Afrika Mashariki.
“Aliamini uandishi wa habari unaofungamana na ukweli na uadilifu ni nguvu kubwa ya wema. Kwa hakika, imani hiyo ilimfanya aanzishe shirika la habari la nyumbani, la kipekee la Afrika Mashariki mwishoni mwa miaka ya 1950,” amesema Jaffer.
Amesema hatimaye ikawa Nation Media Group, ambayo MCL, ni sehemu yake.
Amesema maisha ya Mtukufu Aga Khan IV yalikuwa ushuhuda wa uwezo wa mtu mmoja kubadilisha ulimwengu.
“MCL tunasherehekea urithi wake wa kujitolea. Tunamheshimu kwa kuendelea kutetea uandishi wa habari huru, wa msingi, wenye mwelekeo wa kutafuta suluhu ambao unawawezesha Watanzania kutoka nyanja zote za maisha.
“Kwa moyo huo, tunatumaini tutaendelea kumfanya ajivunie biashara hii kubwa ya vyombo vya habari aliyoianzisha,” amesema Jaffer.
Makamu wa Rais wa Baraza la Taifa la Aga Khan, Nizar Thawer amesema ameshuhudia matokeo ya maono ya Mtukufu Aga Khan kwa watu.
Ameeleza wakati wote wa maisha yake aliwekeza katika elimu, afya na utu wa binadamu.

“Aliamini katika kujenga ujuzi, maisha yake ni mfano bora kwa mamilioni ya watu duniani. Wakati wote alitukumbusha kwamba umoja ni nguvu yetu,” amesema Thawer wakati wa ibada hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Huduma za Afya za Aga Khan Tanzania (AKHST), Amin Habib amesema kifo cha Mtukufu Aga Khan ni pigo kubwa na huzuni kwa Watanzania na mataifa mengine kwa sababu ya kazi kubwa aliyofanya.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Dola 100 milioni za Marekani zilitumika nchini Tanzania kwenye huduma za afya.
“Tutamkumbuka sana, lakini tuna mwendelezo wa uongozi. Tutayaendeleza maono na dhamira yake kwa Tanzania. Tutauenzi ushauri wake wa kuwekeza kwenye afya za watu,” amesema.
Profesa Eunice Pallangyo, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), Mohamed Othman Chande amesema wana furaha kuwa, Mtukufu Aga Khan alikuwa mkuu wa chuo hicho.
Amesema AKU, chini ya usimamizi wake, ilianzishwa miaka 42 iliyopita na kwa Tanzania ilianzishwa mwaka 2002. Amesema jukumu la chuo hicho ni kufanya tafiti na kuzalisha wataalamu.
Amesema wahitimu 1,500 wamemaliza masomo katika chuo hicho.
Profesa Pallangyo amesema zaidi ya Sh2.8 bilioni zimetolewa kwa wanafunzi chuoni hapo, akieleza 900 wamenufaika na mpango huo.
“Baadhi ya wahitimu wa chuo chetu wanashikilia nafasi mbalimbali serikalini na wengine wanaendesha sekta ya afya hapa nchini,” amesema akieleza ushirikishwaji wa jamii ni muhimu.
Amesema maono ya Aga Khan yatabaki kuwa mwongozo wao.
Katika miaka mitano iliyopita, amesema wametekeleza miradi 20 inayoendana na vipaumbele vya Serikali.
Amesema wana machapisho zaidi ya 4,000 yanayochangia kuchochea maendeleo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Diamond Trust Bank (DTB), Ravneet Chowdhury amesema benki hiyo ilianzishwa mwaka 1945 Dar es Salaam kabla ya kusambaa katika mataifa mengine kama Kenya na Uganda.

Amebainisha kwamba, moja ya maono ya Mtukufu Aga Khan IV ilikuwa kujenga umoja katika jamii.
Amesema hilo limejidhihirisha katika benki hiyo ambayo katika wafanyakazi 600 waliopo, wametoka katika mataifa, rangi na dini tofauti.
“Urithi wake haujaandikwa kwa maneno, bali umeandikwa kwenye maisha ya watu aliowagusa. DTB tumejipanga kuendeleza maono yake katika kuhakikisha huduma za afya zinafikiwa,” amesema.
Mwenyekiti wa Bima ya Afya ya Jubilee, Karim Jamal amesema Mtukufu Aga Khan aliwawezesha wananchi wengi kupitia uwekezaji kwenye sekta za elimu, afya na bima.
“Tanzania tumeshuhudia maono yake katika kutengeneza jamii bora na maendeleo ya watu. Aliwekeza katika sekta za afya, elimu, bima na maeneo mengine. Tutaendeleza kazi kubwa aliyoianzisha,” amesema.
Mwenyekiti wa Bima ya Maisha ya Jubilee, Amyn Lalji amesema Mtukufu Aga Khan aliwekeza nguvu zake katika kuleta maendeleo endelevu kwa namna ambayo imeweka viwango vya juu vya kuhudumia jamii.
“Bima ya Maisha ya Jubilee, tuna furaha kuwa sehemu ya maono yake ya kuhakikisha usalama wa kifedha na maisha bora kwa jamii. Tunapotafakari urithi wake wa kipekee, tunatambua jukumu kubwa la kuhakikisha,” amesema Lalji.