Viongozi kampuni wataja mbinu kuepuka utegemezi

Dar es Salaam. Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni (CEOrt-Roundtable), umesema namna pekee ya Tanzania kujiondoa katika utegemezi wa misaada ni kuishirikisha sekta binafsi katika shughuli za kiuchumi.

Viongozi hao wanaowakilisha wakurugenzi wa kampuni zaidi ya 200 nchini wanakuja na hoja hiyo, katikati ya kipindi ambacho Tanzania na mataifa mengine ya Afrika yanakabiliwa na changamoto za huduma kutokana na kukoma kwa baadhi ya misaada kutoka Serikali ya Marekani.

Rais mpya wa Marekani, Donald Trump aliyeapishwa Januari 20, 2025, mapema alitangaza kusitisha misaada mbalimbali kupitia Shirika la Maendeleo la Marekani (Usaid) na mashirika mengine, hali iliyoyaacha mataifa mengi ya Afrika katika mfadhaiko wa kiuchumi.

Hoja ya ushirikishwaji wa sekta binafsi, imeelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt-Roundtable, Santina Benson wakati wa mkutano wa kwanza wa mwaka wenye ujumbe wa ‘Kutenga Jukwa kwa Uchumi Endelevu’ uliofanyika jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana Jumatano, Februari 12, 2025.

Amesema kuishirikisha sekta binafsi katika uchumi wa nchi, kutatua hakikisho la maendeleo na mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

“Ndiyo maana CEOrt imekuwa ikifanya midahalo ili kuwezesha majadiliano juu ya masuala muhimu kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika kutimiza ndoto za Dira ya Maendeleo ya kutoka mwaka 2025 hadi 2050,” amesema.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Santina amesema CEOrt hivi karibuni imezindua mradi wa kuwawezesha wanawake wa Wilaya ya Temeke kiuchumi.

Mradi huo, kwa mujibu wa Benson, unasaidia wanawake wanaojihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kuboresha kipato chao na kukuza uhuru wao wa kiuchumi.

Katika mkutano huo, Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo ameisihi Serikali kuzingatia ukuaji wa uchumi kama msingi wa maendeleo endelevu.

Amesema nchi imepitia mabadiliko magumu ya kiuchumi, kuanzia kwa Hayati Julius Nyerere hadi viongozi waliomfuata, lakini katika kipindi cha hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikishuhudia ukuaji.

Ameongeza katika robo ya kwanza ya mwaka 2007, ukuaji wa uchumi ulikuwa asilimia 11.90 na uliendelea kukua na kufikia asilimia 7.70 mwaka 2011.

Amesema ukuaji huo unatarajiwa kukua na kufikia kati ya asilimia 5.4 hadi 5.7 kwa mwaka huu.

Ametoa wito wa mapitio ya mfumo wa kodi ili uwe rahisi na kuvutia kwa wananchi kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi, ingawa alisema kuwa bado kuna kuna changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma maendeleo ikiwemo rushwa.

Profesa Kinyondo amesisitiza juhudi za Serikali za kubadilisha uchumi zinapaswa kuhusisha sekta binafsi kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika tafiti ili kupata majibu ya changamoto katika sekta mbalimbali hapa nchini.

“Mara nyingi tunategemea wahisani kufadhili tafiti mbalimbali, na baadhi yao huja na masharti yao. Nadhani ni wakati wa Serikali kuanza kufadhili tafiti katika maeneo kama kilimo ili kuleta tija zaidi kwa nchi,” amesema.

Wakati wa mjadala katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Programu ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (Repoa), Dk Donald Mmari ameeleza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii katika kutumia rasilimali zilizopo kuleta maendeleo.

“Tuna rasilimali nyingi ambazo hazijatumiwa ipasavyo ambazo zinaweza kuchukua  jukumu kubwa katika ukuaji wa uchumi,” amesema.

Amesema awali kulikuwa na mikakati ya kukuza uchumi na kupunguza umasikini ‘Mkukuta’ na sasa ni wakati wa kutumia teknolojia kukuza uchumi.