Viongozi kadhaa wazuiwa kuingia kwenye mkutano wa upinzani nchini Angola

Viongozi mbalimbali wa upinzani wakiwemo marais wawili kutoka  mataifa ya Afrika na wengine kutoka kwingineko duniani,  siku ya Alhamisi walizuiwa kuingia nchini Angola kuhudhuria mkutano ulioandaliwa na chama cha upinzani nchini humo UNITA kujadili masuala ya demokrasia.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Ripoti zinasema maafisa wa uhamiaji katika uwanja wa ndege jijini Luanda, waliwazuia wanasiasa wanaokaribia 40 wa upinzani kuingia nchini humo, akiwemo makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo nchini Tanzania.

Wengine waliojipata katika hali hiyo ni Tundu Lissu kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, na Katibu Mkuu wa chama cha ODM nchini Kenya Edwin Sifuna, miongoni mwa wengine.

Rais wa zamani wa Colombia Andres Pastrana aliandika kwenye ukurasa wake wa kijamii wa X kuwa, naye pia alikuwa amezuiwa kuingia nchini humo akiwemo pia na rais wa zamani wa Botswana, Ian Khama na Waziri mkuu wa zamani wa Lesotho.

Serikali ya Angola haijatoa maelezo ni kwanini iliwazuia wanasiasa hao wa upinzani kuingia nchini humo, huku chama cha UNITA kilichoandaa mkutano huo kikilaani kitendo hicho ambacho, kimesema kinachafua jina la nchi na rais Joao Lourenco, ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameendelea kuishtumu Angola kwa kuminya uhuru wa vyama vya upinzani na wanahabari, wanaojaribu kuikosoa serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *