Vilio vyatawala Leaders mwili wa mwigizaji Fredy ukiingizwa

Dar es Salaam.Simanzi na vilio vyatawala viwanja vya Leaders Club baada ya  waombolezaji kushindwa kujizuia mara baada ya kuona mwili wa mwigizaji Fredy Kiluswa ukiwasili viwanjani hapo.

Fredy aliyefariki Novemba 16, 2024 kwa ugonjwa wa moyo anaagwa leo katika viwanja hivyo na kuzikwa makaburi ya  Kinondoni.

                    

Mwili wake umewasili ukiwa umebebwa na wasanii mbalimbali wakiwa wamevalia mavazi ya rangi nyeusi kama ishara ya huzuni ya kumpoteza mpendwa wao.

Kati ya wasanii walioonekana kubeba jeneza la msanii huyo ni Alex Mgeta ‘Ngosha’, Isarito Mwakalindile na wengineo.

                    

Utakumbuka kuwa baba wa marehemu mwigizaji Fredy Kiluswa, Nahum Kiluswa, aliiambia Mwananchi  kuwa kwa mara ya kwanza kijana wake alipata maradhi ya moyo akiwa safarini mwezi mmoja uliopita.

Kiluswa alisema Novemba 16, 2024, Fredy alipozidiwa alikimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwekwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu.

                     

“Hali yake ilikuwa mbaya, alikuwa akipumua kwa shida, huku presha yake ikiwa juu na haikushuka kwa muda mrefu”.
Aliongeza kuwa marehemu hakuwa na historia ya magonjwa hayo hata alipokuwa mtoto.