Mbeya. Wafuasi na makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameendelea kujitokeza ofisi za chama hicho Kanda ya Nyasa ilipo kambi ya kushinikiza kupatikana kwa mwenzao Mdude Nyagali anayetekwa siku 16 sasa bila kupatikana.
Pia, chama hicho kimeeleza kutomtenga mke na familia ya Mdude kikibainisha kinahakikisha kinatoa matumizi kwa watoto na familia kwa ujumla nyumbani kwao.
Mdude alivamiwa na kupigwa nyumbani kwake mtaa wa Iwambi jijini Mbeya na watu wanaosadikiwa kuwa Askari Polisi tangu Mei 2, 2025 ambapo hadi sasa hajapatikana.

Tangu kutokea tukio hilo, viongozi, wafuasi na baadhi ya wananchi waliweka kambi zilipo ofisi za chama hicho Kanda jijini Mbeya wakishinikiza mamlaka kusaidia kupatikana kwake.
Leo Jumamosi, Mei 17 Mwananchi imefika kambini hapo na kushuhudia baadhi ya viongozi kutoka Wilayani Mbarali wakiungana na wenzao kuongeza nguvu kushinikiza Jeshi la Polisi kusaidia kupatikana kwa mwanaharakati huyo.
Akizungumzia kambi hiyo, Katibu wa Chama hicho Kanda ya Nyasa, Grace Shio amesema wameendelea kupokea viongozi na makada kutoka maeneo mbalimbali hali inayowapa nguvu kuendelea kuamini mwenzao kupatikana.
Amesema wanaofika kambini hapo hawaji mikono mitupu, akibainisha hata ugeni uliofika leo kutoka Mbarali, wametua na mzigo wa chakula haswa mchele wa kutosha kusaidia kambi hiyo.
“Hatujaitenga familia ya Mdude, ikiwa ni watoto, mke na wazazi wake tunahakikisha tunawapa matumizi kadri inavyotakiwa huku tukiendelea na kambi yetu,” amesema.
“Tunashukuru watu wanazidi kuungana nasi wakiwamo viongozi wa Chama kutoka mikoani na wilayani na leo wapo kamati tendaji ya Mbarali na hawajaja bure, kuna chakula wameleta mchele mwingi wa kutosha,” amesema Grace.

Katibu huyo ameongeza kuwa kambi hiyo kama walivyoeleza mapema haitakuwa na kikomo hadi pale watakapomuona Mdude akiwa aidha hai au amekufa,” amesema kiongozi huyo.
“Ujio wa wananchi na viongozi inatusaidia kupata mawazo mapya na kuweka mikakati mipya namna ya kupatikana kwa mwenzetu, imani yetu ni kuwa tutampata Mdude akiwa hai,” amesema kigogo huyo.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbarali, Peter Mwashiti amesema ujio wao ni kuongeza nguvu kambini wakilitaka Jeshi la Polisi aidha kumuachia kada huyo au kuongeza juhudi za kumpata alipo.
Amesema baada ya kufika hawana muda rasmi wa kukaa hapo badala yake wanaungana na wenzao kuishi hapo bila kikomo, akieleza kuwa wanaamini Mdude yuko hai na atapatikana.
“Kuja kwetu hatuna muda maalumu wa kukaa hapa, tunasubiri apatikane akiwa hai au amekufa ndio tutaondoka, tumejipanga kuishi hapa kwakuwa tunajichanga na wadau wanatupa sapoti,” amesema.
“Tunaendelea kuwaomba wananchi kuendelea kufichua taarifa za mwenzetu japokuwa tunaamini Polisi wanaye, wadau waendelee kutusapoti tunapokuwa kambini hapa,” amesema Mwashiti.