
Unguja. Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (Zaeca) imesema rushwa imekuwa kikwazo katika mchakato wa uchaguzi na kusababisha kupotea kwa haki za wapiga kura na kuathiri matokeo ya uchaguzi.
Hivyo, mamlaka hiyo imewataka vijana kuwa na ari ya mabadiliko kwa kushiriki kikamilifu katika kampeni za kuelimisha umma, kufichua vitendo vya rushwa na kuhimiza uwazi katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Wito huo umetolewa Jumamosi Aprili 19, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Zaeca, Ali Abdalla Ali katika mkutano maalumu ulioandaliwa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na viongozi wa Mabaraza ya Vijana Zanzibar.
“Hatua hizi hazitaimarisha demokrasia pekee badala yake zitasaidia kujenga taifa lenye misingi imara ya haki na usawa, vijana wanapochukua jukumu hili, wanathibitisha kuwa wao ni nguzo muhimu katika kujenga mustakabali bora wa taifa,” amesema Mkurugenzi Ali.
Amebainisha kuwa vijana ni nguzo muhimu katika kuleta mabadiliko ya kijamii hivyo ni muhimu kujiepusha kutumiwa vibaya na wanasiasa kwa kushiriki katika vitendo vya rushwa, kwani rushwa inaharibu maadili ya jamii na kukwamisha maendeleo ya taifa.
“Mchango wa Vijana ni msingi imara katika kujenga jamii yenye maadili na uwajibikaji, hivyo ushirikiano Wenu ni nyenzo muhimu ya kuhakikisha kuwa rushwa inatokomezwa kabisa hapa nchini,” amesema.
Pia, amewataka vijana kuwa mabalozi kwa kuelimisha wenzao kuhusu madhara ya rushwa na kuhimiza uwazi jambo ambalo litasaidia kufanyika kwa uchaguzi wa haki na bila kuathiriwa na vitendo vya rushwa.
Naye, Katibu Mtendaji Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan alisema katika kuelekea Uchaguzi mkuu Baraza hilo limekuja na kampeni maalumu ya kuhamasisha Vijana na suala la amani inayojulikana kwa jina la ‘amani ni tunu, vijana tuienzi.
Amesema hiyo itasaidia kuhakikisha kuwa rushwa haipati nafasi ya kuathiri maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa nchini.