Vijana watajwa kujihusisha kingono na wanyama

Dar es Salaam. Wadau wa masuala ya afya ya uzazi nchini wamebainisha changamoto zinazowakumba vijana wa rika balehe, ikiwemo kujihusisha kingono na wanyama hususan punda, mbuzi, paka na kuku ili kukidhi matamanio ya kimwili.

Changamoto nyingine ni kujichua kwa vijana wa kiume na wa kike, huku baadhi yao wakibainika kuweka ugoro sehemu za siri kujitosheleza mahitaji ya kihisia.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Novemba 11, 2024 na mratibu wa kuzuia na kupinga ukatili wa kijinsia kutoka Shirika la Norwegian Church Aid, Zaria Mwenge katika mkutano ulioandaliwa na Mtandao wa Taasisi za Kitaifa za Haki za Binadamu Afrika (NANHRI).

“Tulipata ushuhuda kijana alikwenda hospitali akakutwa na maambukizi magonjwa njia ya uzazi hadi wataalamu wakajiuliza wanatibu vipi, lakini kijana alisema amefanya ngono na punda huenda punda naye ana maradhi yake akayabeba ikaja kumletea shida,” amesema.

Zaria amesema matatizo ya watu kufanya ngono na wanyama waliyabaini katika mikoa ya Lindi, Manyara na Wilaya ya Mbulu walipo wafugaji.

Mbali na vijana hao kufanya ngono na wanyama, Zaria amesema wamebaini ndugu kujihusisha kingono, wengine wakiweka ugoro sehemu za siri.

“Wasichana wanakuambia wanatumia ugoro kama njia ya kumaliza haja zao za kimwili, huyu anaingiza ugoro sehemu za siri na huku tunapambana na saratani ya shingo ya kizazi, hili ni tatizo,” amesema.

Zaria amesema ili kukabiliana na changamoto hizo ni muhimu wazazi na jamii kuzungumza na vijana kuhusu mabadiliko ya miili yao na jinsi ya kukabiliana nayo.

Amesisitiza jambo linalorudisha nyuma elimu ya uzazi kwa vijana ni wazazi kutokuwa tayari kuvunja ukimya na watoto wao kuhusu afya ya uzazi.

Kwa upande wake, Eveline Maziku kutoka Wizara ya Afya, idara ya uzazi, mama na mtoto ametaja changamoto inayowakumba vijana balehe ni kutozingatia lishe bora.

 “Vijana vyuoni wanakiri wanakunywa ‘energy’ asubuhi anabaki hana njaa kuanzia muda huo hadi jioni akila hadi kesho tena, hiyo fedha wanabana ili wakanunue simu mpya, Serikali inaendelea na jitihada za kuhamasisha lishe bora,” amesema.

Mbali na hayo, amesema vijana balehe wanakumbwa na changamoto ya afya ya akili, magonjwa ya kuambukiza ikiwemo Ukimwi.

Amesema kwa mwaka 2022 maambukizi mapya ya Ukimwi yalikuwa 60,000 na kupitia takwimu hiyo vijana balehe walikuwa robo tatu.

Naye Joyce Barahuga wa Ofisi ya Rais Tamisemi, Idara ya Elimu anayeshughulikia uzazi salama kwa vijana, amesema katika kukabiliana na changamoto hizo shule za msingi na sekondari wapo walimu wanashughulikia malezi ya wanafunzi.

Pia amesema suala la lishe ya wanafunzi nalo linasimamiwa, kwani Serikali imeagiza shule zote nchini kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni.

Kwa upande wake, Gladness Kirei wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia amesema wizara hiyo imeandaa miongozo mbalimbali, ikiwemo unaohusu stadi za maisha ukilenga elimu ya afya ya uzazi, Ukimwi na jinsia.

“Walimu zaidi ya 5,533 wamepatiwa mafunzo ya namna ya kusaidia vijana, tunaendelea kusambaza miongozo na kutoa elimu kwa walimu namna ya kuwasaidia vijana kwenye masuala ya afya ya uzazi,” amesema.

Kirei amesema tayari mwongozo wa urejeshwaji wanafunzi shule waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali umeendelea kutekelezwa na zaidi ya wanafunzi 22,000 wamerejea masomoni wengi wao waliopata ujauzito.