Vijana, wanawake wafanyabiashara mipakani watakiwa kuchangamkia soko huru Afrika

Arusha. Wanawake na vijana wanaojishughulisha na uuzaji wa bidhaa maeneo ya mipakani, wametakiwa kuzalisha bidhaa zenye ubora ili waweze kushiriki kikamilifu katika soko huru la Afrika linalolenga kuwakwamua kiuchumi.

Aidha katika kukabiliana na vikwazo visivyo vya kiforodha wanavyokumbana navyo, sekta ya umma na sekta binafsi imekutana na vijana na wanawake wanaofanya biashara za mazao ya vyakula mipakani na namna ya kushughulikia vikwazo visivyo vya kiforodha.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Machi 28, 2025 na Mkurugenzi wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Oscar Kisanga akizungumza katika mjadalo huo uliohusisha vijana zaidi ya 100 kutoka mikoa ya Arusha na Manyara, wanaofanya biashara mipakani.

Amesema lengo la majadiliano hayo ni kuinua vijana na kuwapa elimu, ikiwemo za kutambua na kukabiliana na vikwazo pindi wanapofanya biashara zao kwa lengo la kuwahamasisha wachangamkie fursa zilizopo kuanzia soko la ndani hadi la Afrika.

“Lengo ni kuhakikisha makundi haya yanapata fursa ya kujua biashara gani anaweza kufanya na kwa wakati gani, vikwazo atakavyokutana navyo na namna ya kukabiliana navyo.

“Wanawake na vijana ni muhimu mhakikishe mnazalisha bidhaa zenye ubora zinazoweza kushindana katika soko huru Afrika, kama unatengeneza viatu mfano Kariakoo halafu vina viwango vya chini, katika hili soko utawezaje kuuza?

“Tujiandae kuhakikisha hili soko linalokuja tunazalisha bidhaa zenye viwango ili tuweze kuuza bidhaa na kukua kiuchumi,” ameongeza.

Awali, Ofisa Programu kutoka shirika lisilo la kiserikali la Aggra, Donald Mizambwa amesema mjadala huo unafanyika kupitia program ya Youth Entrepreneuship for the Future of Food and Agriculture (Yeffa) ambao wanashirikiana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha wanaleta maendeleo kwenye sekta ya kilimo.

Amesema kupitia programu hiyo vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 wanaofanya biashara katika sekta ya kilimo ikiwemo wanaofanya maeneo ya mipakani kutoka mikoa 18 nchini wananufaika na program hiyo ili kutambua fursa za kiuchumi zilizopo.

Amesema wameungana na Serikali na wadau wengine kuboresha mazingira ya kufanyia biashara katika mipaka ya mikoa ya Mbeya, Songwe, Kigoma, Kagera, Shinyanga, Mara na Arusha kwa kupunguza vikwazo visivyo vya kiforodha.

“Lengo ni kuona vijana wanapata fursa zilizopo sekta ya kilimo lengo mradi ni kuhakikisha asilimia 80 ni vijana wa kike kwani kwa tamaduni nyingi wanawake wanasahaulika na kuoneakana ni wa kufanya shughuli za nyumbani, wakati wanaweza kufanya shughuli za kiuchumi ndiyo maana tunawashirikisha hapa,” amesema.

Mmoja wa washiriki kutoka mkoani Arusha, Vanessa Paul, amesema mafunzo hayo yatawasaidia hasa vijana wa kike kutambua zaidi fursa zilizopo na namna ya kuzitumia katika kukuza uchumi na kuondokana na utegemezi.

“Tunashukuru mjadala huu umetuelimisha masuala mengi ikiwemo kutambua fursa zilizopo nje ya nchi lakini namna ya kuripoti vikwazo vya kibiashara pale tunapokutana navyo na tunaamini tukiwekeza kwenye kilimo tutakuza uchumi wetu binafsi na wa taifa kwa ujumla,” amesema.

Ofisa Biashara wa Mkoa wa Arusha, Njuvaine Mollel amesema kupitia majadiliano hayo wadau hao wakusanye na kuchambua  orodha ya vikwazo na athari zake katika biashara ya mipakani, kutengeneza mipango ya utekelezaji wa kupunguza vikwazo hivyo na kuongeza uelewa wa taratibu za biashara, idhini ya viwango vya biashara na uthibitishaji wa bidhaa za kilimo.

“Niwapongeze wadau wote mnaoendelea kushirikiana na Serikali na tunaahidi kuendelea kusaidia kupunguza vikwazo visivyo vya kikodi vinavyojitokeza ili kuongeza ushirikishwaji wa vijana na wanawake katika biashara za mazao mipakani,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *