
Iringa. Vijana mkoani hapa wametakiwa kuachana na tabia ya kutegemea mahusiano ya kimapenzi kama njia ya kupata unafuu wa maisha kwa wanaume kuwapenda wanawake wenye umri mkubwa zaidi yao, huku wanawake kupenda wanaume watu wazima.
Wito huo umetolewa leo Aprili 30, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Zainab Abdallah ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wakati alipokuwa akihutubia kundi la vijana katika kongamano la vijana, kwenye mbio za mwenge katika Shule ya Msingi Ngome iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ambapo pia Mwenge wa Uhuru, unatarajiwa kukesha katika viwanja hivyo.
DC Zainab amesema kuwa tabia hiyo inawadhalilisha vijana na kuwanyima fursa ya kujitegemea kiuchumi hivyo wanapaswa kujituma na kutumia fursa zinazotolewa na Serikali, kama vile mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vijana, wanawake na makundi maalumu, ili kujikwamua kiuchumi.
“Vijana wa kiume acheni kulelewa na wanawake kwa visingizio vya kutafuta maisha mazuri, tambueni kuwa maisha ya kweli yanahitaji juhudi binafsi na si utegemezi,” amesema DC Zainab
“Mnapopoteza muda kwa mahusiano yasiyokuwa na tija, mnajinyima nafasi ya kuzijua fursa kubwa zinazowazunguka,” ameongeza
DC Zainab amesisitiza kuwa Serikali imeongeza ukomo wa umri wa vijana wanaostahili kupata mikopo hiyo kutoka miaka 35 hadi 45, ili kuwapa nafasi zaidi ya kunufaika nayo.
Katika hotuba yake, DC Zainab amewasihi vijana kuzingatia maadili mema na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuharibu maisha yao, huku akisisitiza kuwa vijana ndio nguvu kazi ya Taifa na wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.
“Tanzania ya leo inahitaji vijana wabunifu, wanaojitambua na wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya nchi kupitia kazi halali na juhudi binafsi,” amesema.
Kongamano hilo limehudhuriwa na vijana zaidi ya 500 kutoka mkoani Iringa na lengo lake ni kuwahamasisha kujituma na kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi, ambapo mada mbalimbali zimefundishwa na wakufunzi kutoka vyuo mbalimbali mkoani Iringa.
Awali kabla ya kufunguliwa kwa kongamano hilo vijana hao wamepatiwa mafunzo mbalimbali ikiwa ni pamoja makuzi na malezi, Afya ya uzazi, fursa za kiuchumi kwa vijana na stadi za maisha na kazi.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Amina Said amesema kuwa baadhi ya vijana hujikuta katika mahusiano ya kimapenzi kwa sababu ya hali ngumu ya maisha, lakini amekiri kuwa ni muhimu kujituma na kutumia fursa zilizopo.
“Sisi kama vijana wa kike tunakumbana na changamoto nyingi, lakini hatupaswi kutegemea uhusiano wa kimapenzi kama njia ya mafanikio,” amesema Amina.
Badru John, mkazi wa Manispaa ya Iringa, amesema kuwa vijana wanapaswa kuacha tabia ya kutegemea wengine na badala yake wajitume na kutumia vipaji vyao kujipatia kipato.
Mmoja wa watoa mada kutoka Chuo Kikuu cha Iringa, Violet Kimbavala ambaye amewasisitiza vijana kuzingatia maadili mema na kuepuka tabia zinazoweza kuharibu maisha yao na pia wajikite katika kuhamasishana wao kwa wao kujituma.
Amesema pia wazitambue na kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi,.