Vijana wabunifu wapigwa msasa

Vijana wabunifu wapigwa msasa

Dar es Salaam. Katika jitihada za kuendeleza na kulinda ubunifu nchini, Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF), kwa kushirikiana na kampuni ya sheria ya NexLaw, imeendesha mafunzo maalumu kuhusu miliki bunifu kwa vijana kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.

Mafunzo hayo yaliyofanyika leo Alhamisi, Mei 22, 2025, jijini Dar es Salaam, yamelenga kuwawezesha vijana kulinda mawazo yao ya ubunifu dhidi ya wizi wa kitaaluma, kuimarisha alama za biashara na kutumia ubunifu kama chanzo halali cha kipato.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Profesa Saudin Mwakaje, mmoja wa wakufunzi wakuu, amesema uelewa wa masuala ya miliki bunifu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa ubunifu na viwanda.

Amesisitiza kuwa elimu hiyo itawawezesha vijana kuvutia wawekezaji, kupanua biashara zao kimataifa na hata kutumia miliki bunifu kama dhamana ya kifedha.

“Mara nyingi vijana wanabuni mambo muhimu, lakini yanapotea kwa kukosa ulinzi wa kisheria. Mafunzo haya yanawaletea maarifa yatakayowasaidia kujilinda na kujiendeleza kibiashara,” amesema Profesa Mwakaje.

Amesema mpango huo unaunga mkono juhudi za Serikali katika kuwawezesha vijana kupata nyenzo muhimu za kujikwamua kiuchumi kupitia ulinzi wa bunifu zao.

Kwa upande wake, mwanasheria kutoka kampuni ya NexLaw, Elizabeth Mlemeta, amesema mafunzo hayo yatawasaidia vijana wabunifu kujua nini cha kufanya endapo wakikumbana na changamoto kuhusu bunifu zao, pamoja na namna ya kudai haki zao.

Baadhi ya vijana wabunifu na wajasiriamali wa kijamii nchini Tanzania wakipata mafunzo maalumu ya kumiliki Ubunifu na ukuaji wa biashara yaliyoandaliwa na Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete (JMKF) yanayofanyika siku mbili jijini Dar es Salaam.Picha na Sunday George

“Vijana wengi hawana uelewa kuhusu haki zao, hali ambayo mara nyingine husababisha migogoro, hasa miongoni mwa wasanii wa muziki,” amesema.

Vijana walioshiriki mafunzo hayo kutoka mikoa mbalimbali wameelezea kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema imewapa mwanga mpya kuhusu thamani ya bunifu zao.

Highness Machange, mbunifu kutoka Mkoa wa Mwanza na mwanzilishi wa kampuni ya Flex Metal inayojihusisha na bidhaa za vyuma, amesema kabla ya mafunzo hayo, alikuwa hajui chochote kuhusu ulinzi wa ubunifu, lakini sasa anaelewa namna ya kusajili nembo na kupata leseni kwa kazi zake.

“Mafunzo haya yamenifungua macho. Nitaenda kushirikisha wenzangu kile nilichojifunza,” amesema Machange.

Akizungumzia mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Maswa Group, Kelvin Steven, amesisitiza umuhimu wa elimu hiyo kwa vijana wabunifu, akieleza kuwa itawasaidia kulinda kazi zao dhidi ya changamoto mbalimbali.

“Hii ni fursa adimu kwa vijana. Itatufundisha kulinda bunifu zisizoshikika kwa ajili ya vizazi vijavyo. Wapo vijana waliopoteza mawazo yao kwa sababu ya kukosa uelewa. Tumepewa zana ya kuanzisha biashara zetu kwa ujasiri zaidi,” amesema Steven.

Ameahidi kuwa balozi wa elimu hiyo kwa kuwafikia vijana wengine ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo.

Aidha, imeelezwa kuwa mafunzo hayo yamechangia kuimarisha misingi ya kisheria inayohitajika kwa ushirikiano wa kimkakati, ubia na mipango ya maendeleo ya muda mrefu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *