
Unguja. Wakati Serikali ikiendelea kuboresha sera na kujenga vituo vya ustadi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Fatma Mabrouk Khamis, amewahimiza vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali ili kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Akizungumza leo Jumatatu Machi 3, 2025, katika mahafali ya kituo cha mafunzo ya vijana huko Unguja, Fatma amesema Serikali ina mpango wa kujenga vituo vya kisasa katika kila mkoa, ili kuwezesha vijana kupata mafunzo mbalimbali yatakayowasaidia kujiajiri na kuimarisha ustawi wao.
Aidha, amesema Serikali imezindua sera mpya ya maendeleo ya vijana ya mwaka 2023, ambayo inalenga kutoa mwongozo kwa wadau katika juhudi za kuharakisha maendeleo ya vijana na kupunguza changamoto ya ajira miongoni mwao.
“Vijana wanapaswa kuwa wabunifu na kutumia mbinu za kisasa, ikiwemo mitandao ya kijamii, ili kuimarisha ujuzi wao na kufanikisha malengo yao,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar, Shaib Ibrahim Muhamed, amebainisha kuwa mafunzo hayo yanawajengea vijana uwezo wa kujitambua kama viongozi bora na kuwawezesha kupata stadi zitakazowasaidia kujiajiri na kuajiriwa.
Pia, amesema vituo hivyo vimeundwa kwa lengo la kuwa na miundombinu rafiki kwa ajili ya kuwapatia vijana mafunzo mbalimbali, yakiwemo ujasiriamali, stadi za maisha, na mafunzo ya uongozi.
Akisoma risala katika mahafali hayo, mwanafunzi wa ushonaji, Asha Ame Mwadini, ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kuanzisha vituo hivyo ambavyo vimekuwa msaada mkubwa kwa vijana.
Hata hivyo, amebainisha changamoto wanazokumbana nazo, ikiwemo ukosefu wa mitaji ya kuanzisha miradi na kuwaomba Serikali, wadau, na watu wenye uwezo kuwasaidia ili waweze kuanzisha miradi yao baada ya kuhitimu mafunzo.
Kituo cha mafunzo ya vijana Bweleo, kilichoanzishwa mwaka 2023 katika Wilaya ya Magharibi B, kimeshatoa mafunzo kwa jumla ya vijana 1,021, wakiwemo wanawake 658 na wanaume 363, katika fani mbalimbali kama stadi za maisha, uongozi, na ujuzi wa kazi.