Vijana hatarini matatizo ya usikivu, chanzo hiki hapa

Dar es Salaam. Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya usikivu leo Machi 3, 2025 takwimu za kidunia zinaeleza kuwa zaidi ya vijana bilioni moja,  wanakabiliwa na hatari ya kupoteza uwezo wa kusikia kabisa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), sababu moja wapo ya changamoto hiyo kwa vijana inatokana na  sauti kubwa wakati wa burudani kama vile kusikiliza muziki au kukaa kwenye mazingira ya kelele kwa muda mrefu.

Mbali na hilo, WHO inasema upotevu wa kusikia huathiri zaidi ya watu bilioni 1.5 duniani kote na kufikia 2050, idadi hiyo inaweza kuongezeka hadi bilioni 2.5.

Vilevile, kufikia 2030, zaidi ya watu milioni 500 wanatarajiwa kuwa na ulemavu wa kusikia unaohitaji matibabu.

Imeelezwa jinsi tutakavyosikia katika siku zijazo inategemea na namna tunavyojali masikio yetu leo, kwani matukio mengi ya  upotezaji wa usikivu,  yanaweza kuepukwa kupitia usikilizaji salama na kujali masikio yetu.

Miongoni mwa dalili za changamoto za upungufu wa kusikia ni kupata ugumu wa kusikia watu wengine wakati wa mazungumzo, kumtaka mtu arudie rudie mara kwa mara, kupata milio ya mara kwa mara kwenye sikio (Tinnitus) sambamba na kusikiliza muziki au televisheni kwa sauti ya juu kuliko kawaida.

Akieleza sababu upungufu wa kusikia na aina ya masikio kupitia mtandao wa Instagram,  Daktari wa masikio pua na koo, Fortunatus Sala anasema,  sikio la binadamu lina sehemu ya sikio la ndani,  kati na nje hivyo changamoto yoyote inayotokea inaweza kusababisha upungufu wa usikivu.

“Aina ya kwanza ya upungufu wa usikivu inaitwa upungufu wa usikivu mwendeshaji inayotokea kwenye sikio la nje au katikati, huku sababu ikiwa ni sikio la nje kujaa nta hivyo sauti kushindwa kufika vizuri.”

Akieleza sababu ya changamoto nyingine amesema inatokana na mgandamizo wa sikio la katikati inayotokea pale sikio linapojaa maji kutokana na sababu mbalimbali. Changamoto ya kimaumbilie kwa sikio la nje au katikati inayosababisha mawimbi ya sauti kushindwa kufika ipasavyo.

“Aina ya pili ni changmoto ya upungufu wa usikivu unaotokana na hitilafu ya umeme inayotokea kutokana na kukaa kwenye mazingira yenye kelele kubwa kwa muda mrefu,” amesema Dk Sala.

Amesema sababu nyingine inatokana na kupata ajali au kuumia eneo la sikio inayoweza kusababisha kupasuka kwa mifupa inayoenda ndani kwenye sikio.

“Changamoto nyingine ni matumizi ya dawa bila ushauri wa daktari zinazoleta athari kwenye sikio la ndani,” ameeleza.

Kwanini vijana

Imeelezwa vijana wako kwenye hatari ya uharibifu wa usikivu kwa sababu ya mambo mbalimbali yanayohusiana na mtindo wa maisha, tabia, na sifa za kifiziolojia.

Miongoni mwazo ni kukaa kwenye mazingira yenye kelele kubwa mara kwa mara, vijana mara nyingi hutumia vichwa vya sauti na vidude vya masikioni (earbuds) kwa muda mrefu wakiwa wameongeza sauti wakati wa kusikiliza muziki, kutazama video au kucheza michezo ya video.

Aidha kuhudhuria matamasha yenye kelele kubwa, vilabu vya usiku na matukio ya michezo, huongeza hatari ya kupoteza usikivu unaosababishwa na kelele.

Pia vijana wengi hawatambui kuwa uharibifu wa usikivu ni wa kudumu na huweza kuongezeka polepole kwa muda.

Kupoteza usikivu kwa vijana kunaweza kusababisha changamoto katika mawasiliano, upweke wa kijamii, na matatizo ya kitaaluma.

Namna ya kulinda masikio yako

Kitaalamu imeelezwa ili kulinda masikio unapaswa kuweka sauti chini ya asilimia 60 au utumie vifaa vya kupokea sauti vinavyovaliwa kwa kubanwa kichwani kwaajili ya kupunguza kelele.

Kuvaa kinga ya masikio, kama vile viziba masikio, kwenye matamasha na sehemu za kazi zenye kelele.

Kauli mbili ya maadhimisho ya mwaka huu inasema: Kubadilisha mawazo: Jiwezeshe kufanya huduma ya sikio na kusikia kuwa ukweli kwa wote! Unaweza kuchukua hatua leo ili kuhakikisha afya nzuri ya kusikia katika maisha yote.

Asemavyo kijana

Kijana Amani Yohana kutoka Dar es Salaam anasema kwa upande wake hapendi kusikiliza muziki kwa sauti kubwa sababu naelewa kufanya hivyo naweza kuharibu uzima wa masikio yake.

“Kwani baadhi ya watalaam wanasema kusikiliza mziki kwa sauti kubwa naweza kuharibu ngoma ya sikio, hio ndio sababu ya mimi kupenda kusikiliza muziki kwa sauti ndogo,” amesema.