Vigogo watangaza kung’oka Chadema, wakidai kinaendeshwa bila kufuata katiba

Dar es Salaam. Wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaounda kundi la G55 wamekutana leo Jumatano, Mei 7, 2025 wametangaza kuondoka ndani ya chama hicho kwa sababu kimeshindwa kufuata malengo ya kuanzishwa kwake.

Uamuzi huo wameutangaza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwa madai wamechoshwa na jinsi chama hicho chini ya uongozi wa Tundu Lissu kilivyoshindwa kuishi misingi ya kuanzishwa kwake.

Wanachama hao walioshiriki mkutano huo, wamevalia nguo nyeupe wote. Miongoni mwa waliopo kwenye mkutano huo ni Julius Mwita, John Mrema, Catherine Ruge, Salum Mwalimu ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila amesema hali ya kisiasa ndani ya chama hicho imegubikwa na kile alichokiita ‘ubaguzi mkubwa’ dhidi ya wanachama wanaohusishwa na upande wa Freeman Mbowe, ambao wamekuwa wakitengwa kuanzia ngazi ya kamati Kuu hadi mashinani.

Kigaila amesema licha ya Mbowe kutoa wito wa kuvunjwa kwa makundi na kuundwa kwa kamati ya maridhiano baada ya uchaguzi wa chama, ushauri huo uligonga mwamba mara moja mbele ya wajumbe.

“Wakati anazungumza Freeman Mbowe baada ya uchaguzi, alitoa ushauri kwenye chama kuvunja makundi, kukiunganisha chama na kuunda kamati ya maridhiano ili chama kiweze kurudi pamoja kupigania haki, utu na maendeleo ya watu. Lakini mwenyekiti aliyeshinda alimshutumu Mbowe palepale mbele ya wajumbe,” amesema Kigaila.

Kwa mujibu wa Kigaila, matokeo ya hali hiyo yamekuwa ni kuendelea kwa ubaguzi wa wanachama wanaojulikana kuwa walimuunga mkono Mbowe, ambao sasa wanatengwa waziwazi.

“Kila mtu anayejulikana kwamba alimuunga mkono Mbowe anaitwa msaliti. Hali hii imeenea kuanzia Kamati Kuu hadi kwenye misingi ya chama,” ameongeza Kigaila.

Baada ya kueleza kwa kina yanayoendelea Chadema, Kigaila amesema: “Sisi tumeamua wote pamoja tunajiondoa Chadema ili tuwaachie waendeshe wanavyotaka. Sisi hatuwezi kuwa wanachama wa chama ambapo uamuzi wake haufanywi kwa vikao, hatuwezi kuwa wanachama ambao tunabaguliwa, katiba haifuatwi.”

“Tuliingia Chadema kwa malengo na kwa sababu malengo yameisha basi tunawaachia chama chao,” amesema.

Kigaila amesema kwa sasa bado wanafanya mawasiliano na vyama mbalimbali: “Tunatafuta jukwaa muafaka la kwenda kuwatumikia Watanzania kwa sababu hatujazeeka, tunaondoka leo Chadema tunaenda kutafakari tutaenda chama gani, lakini mjue CCM si mbadala wetu ila tutawaambia ni wapi tunakwenda.”

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Zanzibar, Salum Mwalimu amesema anaungana na Kigaila kukihama chama hicho kwa kuwa kila wakijaribu kuushauri uongozi uliopo hoja yao ni No reforms, no election.

“Nimekaa Chadema miaka 17, nashauri hawanisikilizi kila nikiwafuata ni No reforms, no elections, sasa sisi ni watu wazima, tumevumilia tumechoka ndani ya Chadema hakuna kinachoendelea,” amesema

Amesema ndani ya Chadema kuna anguko tena la makusudi na kutaka kuzima ndoto na matumaini ya watu wengine.

“Kwenye vikao wamekuwa wanaangaliana wewe ni No reforms, no election, kama si mlengo huo unatengwa, haiwezekani tubaki Chadema kwa mazingira ya namna hiyo,” amesema

Amesema muda utaongea huku akiwataka wengine kuwaunga mkono katika kuhama.

“Haya yote ni matokeo ya udhaifu wa uongozi uliopo madarakani, chama kinaendeshwa kwa matamko hawazungumzi lugha moja.”

“Natangaza rasmi uanachama wangu ndani ya Chadema unakoma, hakuna cha kuogopa naenda kuendeleza taranta yangu sehemu nyingine,” amesema Mwalimu.

Akizungumza kwenye mkutano huo, aliyekuwa Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Catherine Ruge amesema “Siku zote naamini Chadema ilisajiliwa kwa ajili ya kushika dola na kutatua matatizo makubwa ya msingi.

“Lakini leo Chadema niliyoitumikia kwa jasho langu la damu ndani ya miaka 15 na hakuna anayeweza kubeza, badala ya kubuni mbinu ya kuwapa matumaini wananchi namna ya kuikabili CCM matokeo yake wanawatia hofu Watanzania.”

“Niliwahi kushauri lakini sikuzingatiwa mimi siwezi kuwa kwenye chama ambacho siamini kwenye ajenda na msimamo leo nimeamua kuachana na Chadema rasmi,”amesema Ruge.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *