
Michuano ya Klabu Bingwa Ulaya ‘UEFA Champions League’ iliendelea tena usiku wa kuamkia leo ambapo viwanja tisa vilikuwa vikitimua vumbi huku Arsenal na PSG zikishidwa kutamba.
Arsenal ilikuwa ugenini kwenye Uwanja wa San Siro dhidi ya Inter Milan ambapo ilikubali kipigo cha bao 1-0 lililofungwa na Hakan Çalhanoğlu mwishoni mwa kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penalti baada ya kiungo wa Arsenal Mikel Merino kushika mpira kwenye eneo la hatari.
Arsenal inaruhusu bao la kwanza baada ya kufungwa na Inter Milan ambapo ilikuwa haijapoteza wala kuruhusu nyavu zake kutikiswa katika mashindano haya.
Hili ni bao la kwanza Arsenal inaruhusu kwenye michuano hii mwaka huu baada ya awali kucheza mechi tatu bila kupoteza mchezo au kufungwa bao.
PSG ilishindwa kutamba nyumbani dhidi ya vijana wa Diego Simeone Atletico Madrid walipokubali kipigo cha mabao 2-1 huku Angel Correa akiifungia Atletico bao la ushindi dakika za mwishoni mwa mchezo.
Barcelona chini ya kocha wake Hansi Flick imezidi kutamba baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 5-2 walipokuwa ugenini dhidi ya Crevena Zvezda ya Serbia huku Robert Lewandowski akifunga mabao mawili na mengine yakifungwa na Raphinha, Martinez pamoja na Lopez.
Bayern ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa na Barcelona ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Benfica, Stuttgart walipoteza nyumbani 2-0 dhidi ya Atalanta, Brest ilishinda ugenini 2-1 dhidi ya Sparta Prague, Feynoord ilipoteza nyumbani 3-1 dhidi ya RB Salzburg, Shakhtar Donetsk ilishinda nyumbani 2-1 dhidi ya Young Boys, wakati Aston Villa wakipoteza ugenini 1-0 dhidi ya Club Brugge.
Baada ya michezo hii makocha mbalimbali wamekuwa wakilalamika kuwa wachezaji wao wamechoka kutokana na kucheza michezo mingi kwa muda mfupi.