Vigogo hesabu tofauti Europa

Nyon,Switzerland. Hatua ya ligi ya mashindano ya Kombe la Europa inafikia tamati leo huku vita ya kuwania nafasi nane za kutinga hatua ya 16 bora bila kutegemea mechi za mchujo kusaka nafasi nyingine nane ikionekana kuzipa mvuto mechi 18 zitakazochezwa katika viwanja na miji tofauti.

Tayari Lazio imejihakikishia nafasi moja kati ya nane za kutinga moja kwa moja hatua ya 16 bora bila kucheza mechi za mchujo kwa vile inaongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 19 ambazo zitaifanya imalize ikiwa miongoni mwa timu nane ambazo zitafuzu moja kwa moja hatua inayofuata.

Shughuli pevu ipo kwa timu 14 ambazo zinawania nafasi saba ziliazobakia na ikiwa itashindikana, zitalazimika kutafuta tiketi ya kutinga hatua ya 16 bora kupitia mechi za mchujo.

Matokeo ya sare yatakuwa na maana kubwa kwa Eintracht Frankfurt na Athletic Bilbao leo kwani yatazifanya kila moja kufikisha pointi 17 ambazo zinatosha kuzifanya zimalize katika kundi la timu nane za juu kwenye ligi hiyo.

Franfurt itakuwa ugenini kukabiliana na AS Roma na Athletic Bilbao itakuwa nyumbani kucheza na Viktoria Plzeň.

Ushindi ni matokeo yanayohitajika vilivyo na Manchester United katika mchezo wake wa ugenini dhidi ya FCSB ili ifikishe pointi 18 ambazo zitaifanya iungane na Lazio ambaye imeshatangulia katika hatua ya 16 bora.

Matokeo ya sare yanaweza kuibeba Man United na kuipeleka katika hatua inayofuata ikiwa tu Plzen na Olympiacos ambazo kila moja ina pointi 12 hazitoweza kupata ushindi katika mechi zao za leo.

Wakati Plzen ikikabiliana na Athletic Bilbao, Olympiacos yenyewe itakuwa nyumbani kucheza na Qarabag.

Ukiondoa Man United, timu za Olympique  Lyon, Tottenham Hotspur na Anderlecht zitajihakikishia tiketi ya kutinga hatua inayofuata ikiwa kila moja itapata ushindi kwenye mechi yake ya leo.

Spurs itakuwa nyumbani kukabiliana na Elfsborg, Lyon itaikaribisha Ludogorets na Anderlecht itaialika TSG Hoffenheim.

Mbali na mechi hizo, nyingine leo ni kati ya Ajax na Galatasaray, Dinamo Kiev na Rigas FS, Midtjylland dhidi ya Feberbahce, Twente itacheza na Besiktas, Ferencvaros itaikaribisha AZ Alkmaar na Maccabi Tel Aviv itakabiliana na Porto.

Pia Nice itaialika Bodo/Glimt, Rangers itaikaribisha Union Saint-Gilloise, Real Sociedad dhidi ya PAOK, Slavia Prague itacheza na Malmo na Sporting Braga itakuwa nyumbani kucheza na Lazio.