Vigogo Championship wahamishia nguvu FA

BAADA ya kushuhudia Mbeya City ikiwa timu ya kwanza ya Championship kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), miamba wengine watatu waliobaki katika mashindano hayo watashuka kwenye viwanja mbalimbali kusaka pia tiketi hiyo.

Stand United iliyoichapa Fountain Gate kwa penalti 4-3, baada ya sare ya 1-1, itakuwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga Jumatano ya Machi 26, kucheza na Mabingwa wa Mkoa wa Katavi, Giraffe Academy iliyoitoa Green Warriors kwa bao 1-0.

Bigman FC iliyoitoa Tanzania Prisons kwa penalti 3-2, baada ya sare ya bao 1-1, itakuwa na kibarua kigumu cha kupambana na Simba iliyoichapa TMA ya Arusha mabao 3-0, mchezo utakaopigwa Alhamisi hii ya Machi 27, kwenye Uwanja wa KMC Complex.

Timu ya mwisho ni Songea United iliyoitoa Polisi Tanzania kwa bao 1-0, itakayopambana na mabingwa watetezi wa michuano hiyo Yanga iliyoichapa Coastal Union mabao 3-1, mechi itakayopigwa Jumamosi ya Machi 29, kwenye Uwanja wa KMC Complex.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, kocha wa Bigman FC, Zubery Katwila alisema wanatambua wanaenda kukutana na timu bora na yenye wachezaji wazuri, ingawa wamejipanga kuhakikisha wanaleta ushindani kama walivyofanya katika hatua zilizopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *