Vigogo Afrika katika njia ya Yanga Ligi ya Mabingwa

Dar es Salaam. Yanga imeendelea kupeperusha vyema bendera ya Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya Jumamosi iliyopita kuibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya CBE ya Ethiopia kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.

Matokeo hayo yameifanya Yanga ifuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa mabao 7-0 katika mechi mbili baina ya timu hizo baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza huko Ethiopia, Septemba 14.

Kabla ya hapo, Yanga iliitoa Vital’O ya Burundi kwa ushindi wa mabao 10-0 ikishinda mabao 4-0 katika mechi ya kwanza na kisha ikapata ushindi wa mabao 6-0 katika mechi ya pili.

Kufuzu hatua ya makundi ni ishara tosha ya harakati za Yanga kusaka Ufalme wa Afrika kwa maana ya kuwania taji la ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, kutwaa ubingwa wa mashindano hayo msimu huu huenda lisiwe jambo rahisi kwa Yanga na hiyo ni kutokana na sababu mbalimbali.

Vigogo mfupa mgumu

İli ndoto yake itimie Yanga inapaswa kujipenyeza katikati ya timu takribani saba zenye historia kubwa ya kufanya vizuri katika soka la Afrika ambazo nazo zimefanikiwa kuingia hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Uwepo wa timu hizo ambazo pia zinasifika kwa uwekezaji ambao zimefanya katika kusuka vikosi vyao na pia katika kujiendesha kwao katika mashindano mbalimbali zinazoshiriki.

Ahly ya Misri ndio tishio kubwa kwa Yanga kwani ndio timu yenye historia nzuri ya kuwa na muendelezo wa kutamba katika mashindano hayo lakini pia ndio klabu ghali zaidi hapa Afrika.

Timu hiyo ya Misri ndio inashikilia rekodi ya kutwaa mara nyingi zaidi taji la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa imelichukua mara 12 lakini pia imechukua mara nane, taji la Caf Super Cup ambalo hutwaa timu inayoibuka mshindi katika mchezo unaokutanisha bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika na Bingwa wa Kombe la Shirikisho.

Kwa mujibu wa mtandao wa Transfermrk, Al Ahly kikosi chake kina thamani ya Euro 28.4 milioni (Sh86.5 bilioni) na hivyo kuwa klabu ya pili kwa kuwa na kikosi chenye thamani kubwa zaidi baranı Afrika, kinara ikiwa ni Mamelodi Sundowns.

Timu nyingine ukiondoa Al Ahly ni Raja Casablanca, Esperance, Mamelodi Sundowns, TP Mazembe na Orlando Pirates.

Hata hivyo, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ametamba kwamba timu yake haina hofu dhidi ya mpinzani yoyote na iko tayari kukabiliana na timu yoyote ambayo watapangwa nayo.

“ Yanga sisi ni timu kubwa hatuwezi kuogopa timu yoyote ila tutaziheshimu tu. Naenda kucheza na kushindana nazo uso kwa uso kwenye makundi,. Yanga inapaswa kupewa heshima kwenye soka la Afrika,” alisema Gamondi.

Noti zaongeza morali

Kiasi kikubwa cha fedha ambazo timu zinavuna kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia hatua ya makundi hadi fainali hapana shaka zinaongeza hamu na shabaha ya Yanga kufanya vizuri zaidi katika mashindano hayo.

Kadri timu inavyosogea hatua ya juu zaidi katika mashindano hayo ndivyo inavyovuna fedha nyingi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).

Kitendo cha kutinga tu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kinaihakikishia timu kiasi cha Dola 700,000 (Sh 1.8 bilioni) na ile inayoingia hatua ya robo fainali inavuna Dola 900,000 (Sh 2.3 bilioni).

Bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika anapata kiasi cha Dola 4 milioni (Sh10 bilioni),  mshindi wa pili anapata kitita cha Dola 2 milioni (Sh 5 bilioni) na inayoishia nusu fainali inapata Dola 1.2 milioni (Sh3.2 bilioni).

Ukiondoa fedha hizo za Caf, noti nyingine ambazo Yanga itakuwa inaziwinda ni zile zinazotolewa kama bonasi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia hutoa kiasi cha Sh5 milioni kwa kila bao linalofungwa na klabu ya Tanzania inayoshiriki mashindano ya klabu Afrika.

Kwa raundi mbili tu ambazo imecheza kabla ya hatua ya makundi, Yanga imeshavuna Sh85 milioni kutoka kwa fungu hilo la fedha la Rais Samia lijulikanalo kama bao la mama.

Yanga ilivuna Sh50 milioni kwa kupata mabao 10 dhidi ya Vital’O kwenye raundi ya kwanza na Sh35 milioni kwa mabao saba iliyoyapata dhidi ya CBE.

Deni la miaka 59

Ni fursa muhimu kwa Yanga kuhitimisha unyonge wa miaka 59 ambao imekuwa nao kwenye mashindano ya klabu Afrika ikiwa itafanya vizuri zaidi msimu huu.

Unyonge huo ni wa kutowahi kutinga angalau hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo tangu yalipoanzishwa rasmi mwaka 1965.

Mafanikio makubwa kwa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni kutinga hatua ya robo fainali ikifanya hivyo mwaka 1969 na 1970 pamoja na msimu uliopita.

Mwaka 1969 ilitolewa na Asante Kotoko ya Ghana kwa uamuzi wa kurusha shilingi baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 na mwaka 1970 ilitolewa tena na timu hiyohiyo kwa kufungwa mabao 3-1.

Msimu uliopita ilitolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penaltı 3-2 baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya bila kufungana.

Ndoto zinaishi

Beki na nahodha msaidizi wa Yanga, Dickson Job alisema kuwa lengo lao kuu ni kufika hatua za juu za mashindano hayo na ikiwezekana kutwaa ubingwa.

“Msimu uliopita ilibaki kidogo tuingie nusu fainali na kwa bahati mbaya tukatolewa katika mazingira ambayo kila mmoja aliyaona. Kile kilichotokea dhidi ya Mamelodi Sundowns kilituimairisha na kutukomaza zaidi.

“Kwa sasa naweza kusema hakuna timu ambayo tunaihofia na tunaamini tukijipanga na uongozi pamoja na mashabiki wakiendelea kutupa sapoti tutapata mafanikio makubwa msimu huu,” alisema Job.

Kipa Abubakar Khomeiny alisema ubora wa kikosi walichonacho unawapa matumaini ya kutimiza malengo waliyoweka kimataifa.

“Hakuna ambacho kinashindikana kwenye soka kama wote mnakuwa na malengo ya pamoja na kila mmoja anajitolea kuhakikisha kile ambacho timu imekipanga kinatimia.

“Kwa kikosi tulichonacho, ubora wa benchi letu la ufundi chini ya kocha Miguel Gamondi pamoja na uongozi wa Rais wetu Hersi (Said), naamini malengo yetu yatatimia.

Timu zilizofuzu 16 Bora Ligi ya Mabingwa:

Al Ahly, Espérance, Mamelodi Sundowns na TP Mazembe zipo poti namba moja, poti namba mbili zipo CR Belouizdad, Raja CA, Yanga na Pyramids poti namba tatu zipo timu za Al Hilal, Orlando Pirates, Sagrada Esperança, AS FAR huku namba nne zikiwemo MC Alger, AS Maniema, Stade d’Abidjan na Djoliba.