
Dar es Salaam. Vikao vya kuhitimisha uhai wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vinatarajiwa kutamatika Juni 27, 2025.
Katika kipindi hiki, wabunge wanaotarajia kutetea nafasi zao wanakabiliwa na mitihani mitano mikubwa, ikiwemo kujenga ushawishi miongoni mwa wajumbe wa vyama vyao ili kulinda kura walizovuna mwaka 2020 na kuongeza mpya.
Changamoto nyingine ni ushindani kutoka kwa watia nia wapya, hali ya uhusiano wao na wananchi, migogoro ya ndani ya vyama vyao, pamoja na uwezo wa kutimiza matarajio ya wananchi.
Watakaofanikiwa kuvuka vigingi hivi wana nafasi kubwa ya kurejea bungeni na kuendelea kunufaika na maisha ya kibunge.
Safari ya Bunge hili, ambalo limetawaliwa na wabunge kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), ilianza rasmi Novemba 2020, kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huo.
Bunge lilizinduliwa Novemba 13 na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, aliyefariki dunia Machi 17, 2021.
Uchaguzi uliowavusha baadhi ya wabunge kuingia bungeni uligubikwa na hisia mseto kutoka vyama vya upinzani, ambavyo mara kwa mara vilidai kuwa haukuwa wa haki na haukutoa uwanja sawa wa ushindani.
Sasa, duru mpya ya kinyang’anyiro hicho cha kisiasa inaanza kuchukua nafasi yake tena mwaka huu.
Katika kutafakari mustakabali wa wabunge wanaomaliza muda wao, kuna taswira pana ya changamoto na fursa zinazochangia ongezeko la ushindani.
Tayari dalili za mabadiliko ya mwelekeo wa kisiasa zimeanza kuonekana kabla ya kuvunjwa rasmi kwa Bunge hilo hapo Juni 27, 2025.
Watia nia wapya wenye mvuto na nguvu ya ushawishi wameanza kujitokeza majimboni, wakijinadi kwa wananchi kwa kasi, wakionyesha nia ya kuwania nafasi hizo, japokuwa kipyenga bado hakijapulizwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Wengine miongoni mwao wanapata uungwaji mkono kutoka kwa wajumbe wa kamati za siasa na viongozi wakubwa wa vyama wenye uwezo kifedha, hali inayowaweka katika nafasi nzuri ya kuwania nafasi hizo kwa mafanikio.
Baadhi ya wabunge wameanza kuingiwa na hofu, wakipokea jumbe zisizotia moyo kutoka kwa wapigakura wao, zikihimiza waache kutapanya fedha walizopata wakati wa ubunge na badala yake waandae maisha mapya baada ya kutoka bungeni.
Wapo hata wananchi waliodiriki kuchapisha fulana zenye ujumbe unaosomeka: “Miaka mitano inatosha, tupeni mwakilishi mpya atakayetuvusha.” Hii inaonyesha mabadiliko ya mitazamo ya wapigakura.
Kwa sababu ya ongezeko la joto la kisiasa kutoka mitandao ya kijamii hadi uhalisia wa maeneo ya majimbo, kuna matarajio kuwa baadhi ya wabunge watakwepa kuhudhuria vikao vya mwisho vya bunge vinavyolenga kupitisha bajeti ya mwaka ujao wa fedha, na wanachanja mbuga majimboni kusaka huruma ya wananchi.
Ingawa baadhi yao wamejitokeza hadharani kuomba msaada kwa viongozi wa vyama vyao kuwadhibiti wanachama wanaowasumbua, bado onyo na maelekezo kutoka juu yanaonekana kutoleta athari yoyote ya mabadiliko wala utulivu majimboni.
Uhusiano wao na wananchi
Akiizungumzia hoja ya uhusiano wa mbunge na wananchi, mchambuzi wa siasa, Adolf Kwame anasema mbunge anapaswa kutambua kuwa uhusiano mzuri na wananchi ni sehemu muhimu ya mafanikio yake katika siasa.
Kwame anasema kama mbunge alikuwa na uhusiano mbaya na wananchi, itakuwa vigumu kwake kuendelea kushikilia nafasi hiyo kwa muhula mwingine.
“Mbunge anaposhindwa kujenga na kudumisha uhusiano mzuri na wapigakura wake, kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza uungwaji mkono wao, na hii inaweza kumpelekea kushindwa katika uchaguzi ujao. Uhusiano mzuri unajenga heshima na uaminifu kwa mbunge,” anasema Kwame.
Anasema wananchi wanapomwona mbunge anayehusika na maendeleo ya jamii, wanapata motisha ya kumchagua tena.
Lakini ambaye hana uhusiano mzuri wanamtafasiri kuwa alikuwa hana muda na magumu wanayokabiliano nayo na hakuweza hata kuwasemea bungeni katika kipindi chote cha miaka mitano.
“Wananchi wengi kwa sasa wajanja, wanajua haki zao, wanahitaji kuona mbunge anayewajali na anashughulikia matatizo yao,” anasema.
Mahitaji ya wananchi
Siku zote wananchi wanahitaji viongozi wenye maadili, uaminifu na uwezo wa kufanya uamuzi bora kwa maslahi yao.
Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu, Wakili Anna Henga, anasema wananchi wanahitaji viongozi wenye weledi, uongozi bora, na dhamira ya kweli ya kuwatumikia watu wao kwa manufaa ya jamii nzima.
Henga anasema kutokana na hilo, ni wazi kuwa wananchi hivi sasa lazima watampima mbunge kama alikuwa anawajali au alitekeleza kila jambo kwa maslahi ya kundi fulani au yeye binafsi au jamii nzima jimboni kwake. “Mbali na hilo, wananchi wanataka wagombea ambao wana rekodi ya utendaji bora katika nyanja mbalimbali, iwe ni katika utawala, shughuli za kijamii, au biashara. Ufanisi katika maeneo haya husaidia kujenga imani kwa wagombea,” anasema kiongozi huyo.
Hata hivyo, anasema jambo la msingi wanalotakiwa kufanya sasa, ni kuonyesha wamefanya nini kwa miaka mitano ambayo Watanzania wamewapa dhamana.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya kijamii na siasa Tanzania, Profesa Ambros Kessy anasema ni dhahiri mazingira ya kisiasa yamebadilika kwa kasi, hasa kutokana na kuongezeka kwa watiania wapya ambao wamezindua harakati za kujitambulisha mapema na kuonesha dhamira ya kuwania nafasi hizo. Hali hii inawapa wabunge waliopo mizigo miwili mikuu,” anasema.
Akifafanua mizigo hiyo, Profesa Kessy anasema kwanza kuhakikisha kazi zao za awali zinajitokeza kama nguzo thabiti ya kukubalika tena na kutafuta mbinu mpya za kukabiliana na msukumo wa kisiasa unaojengwa na wapinzani walio na mbinu mbadala za kujinadi majimboni.
“Wagombea wanaowania nafasi za uwakilishi katika Bunge mara nyingi hukumbana na vikwazo vinavyotokana na kupungua kwa imani ya wapigakura, hasa pale penye hitilafu kati ya ahadi walizotoa awali na utekelezaji wake. Kwa hiyo, changamoto kuu ya kwanza inayojitokeza ni shinikizo la uwajibikaji,” anasema.
Anasema wabunge hao wanahitaji kuonekana wamewajibika katika miaka yao ya uongozi, wakidhihirisha wamewezesha miradi ya maendeleo, wamesimamia matumizi bora ya rasilimali na kushirikisha wapigakura katika mchakato wa kufanya uamuzi.
“Endapo wapigakura watatafsiri utendaji wao kuwa haujakidhi matarajio, basi watia nia wapya watakuwa na hoja nzito za kuonyesha namna watakavyoziba pengo hilo,” anasema.
Changamoto ya pili, Profesa Kessy anasema inahusiana na utandawazi wa habari na mitandao ya kijamii.
“Katika nyakati zilizopita, mbunge angeweza kutegemea mikutano ya hadhara na mahusiano ya karibu na viongozi wa kimila au wa dini kujenga umaarufu,” anasema Profesa Kessy na kuongeza:
“Hata hivyo, leo hii taarifa kuhusu utekelezaji wa ilani za uchaguzi, maamuzi tata, au masuala yanayohusiana na uadilifu wa viongozi, husambaa kwa kasi kupitia majukwaa ya kidijitali.”
Profesa Kessy anasema kuna mtazamo wa jumla katika jamii kuwa na hali ya kuchoshwa na kuwaona wanasiasa walewale kila kipindi cha uchaguzi.
“Mara nyingine wapigakura hupendelea kuona sura mpya zinazoleta mitazamo mipya katika kushughulikia changamoto za kijamii na kiuchumi katika maeneo yao. Kwa hiyo, iwapo mbunge hawezi kuwasilisha mawazo mapya ya maendeleo, iwe ni katika vikao vya jimbo au bungeni, basi hana budi kujiandaa na mabadiliko,” anasema.
Anaeleza kuwa kama wabunge waliopo hawatabadilisha mbinu zao za kujinadi wala kuboresha mikakati ya kutatua matatizo ya wananchi, basi wanakabiliwa na hatari ya kuchukuliwa kama watu wasiokuwa na mchango mpya.
Kwa mujibu wa Profesa Kessy, ni muhimu kwa wabunge waliopo kuonyesha uwezo wao wa kubuni mikakati mipya ya kisera na hatua za vitendo.
Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, anasema kuna hatua kadhaa ambazo wanaweza kuchukua ili kulinda nafasi zao. Kwanza, ni kwa kuimarisha uwazi na ushirikishwaji wa wananchi.
“Kwa mfano, kuandaa mikutano shirikishi ambayo siyo tu ya kisiasa, bali pia iwe ni jukwaa la majadiliano ya dhati kuhusu utekelezaji wa ahadi zilizopita. Pili, matumizi ya mitandao ya kijamii yanapaswa kuimarishwa ili kutoa mrejesho na kueleza mipango inayofuata,” anasema.
Anaongeza kuwa hatua hizi zinaweza kusaidia kupunguza pengo la mawasiliano kati ya viongozi na wapigakura.
Pia anasisitiza umuhimu wa wabunge kujenga mtandao mpana wa kisiasa kwa kushirikiana na wadau kama viongozi wa kijamii, asasi za kiraia, na wananchi wenyewe katika kutambua na kutatua masuala muhimu.
“Wadau hawa wana ushawishi mkubwa katika kulinda taswira ya kisiasa ya kiongozi,” anasema.
Naye Dk Richard Mbunda, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema uchaguzi wa mwaka 2025 unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa pamoja na matumizi ya fedha kwa kiwango kikubwa, kutokana na kuongezeka kwa ushiriki wa wapigakura wa ndani.
“Baadhi ya wagombea wanaweza kupoteza nafasi zao kwa sababu hawakujipanga vyema, hasa katika kukabiliana na changamoto za ndani ya chama,” anasema Dk Mbunda.
Anaeleza kuwa kuna changamoto nyingine kutoka nje, hasa iwapo chama cha Chadema kitaamua kushiriki uchaguzi endapo kampeni yao ya “No Reforms, No Election” itafikia mwisho.
“Kigezo muhimu cha kuchaguliwa tena ni jinsi gani mbunge alijitahidi kuwatetea wananchi wake bungeni. Lakini kutokana na kutokuwepo kwa kambi rasmi ya upinzani, wabunge wengi hawakuweza kufanya vizuri. Hii inaweza kuwagharimu, na wakatafsiriwa kama watu waliokuwa wa kufuata mkumbo tu,” anasema Dk Mbunda.
Ushawishi wa wajumbe
Kwa mfano, Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatumia mfumo wa kuwashirikisha wajumbe wa wilaya, ambao wamepewa mamlaka kwa mujibu wa Katiba ya chama, ili kuchagua wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge kupitia kura za maoni.
Mfumo huu ni njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki moja kwa moja katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wao katika maeneo husika. Hii inawataka wabunge waliopo na watakaojitokeza kuwania nafasi hizo, kujenga hoja zenye mvuto mkubwa ili kuwashawishi wajumbe wawape kura na kuwapa uungwaji mkono.
Kwa mujibu wa CCM, katika uchaguzi wa mwaka huu, hata kama watiania wa kugombea jimbo moja watakuwa 70, mchujo utafanyika na majina ya wagombea watatu waliopata kura nyingi zaidi kutoka kwa wajumbe yatapelekwa kwa ajili ya uteuzi.Mgombea atakayepata kura nyingi na kuonekana anaungwa mkono kwa wingi na wananchi ndiye atakayeteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho.
Mfumo huu unawapa wajumbe nafasi ya kipekee na ya muhimu katika mchakato wa uchaguzi huo. Hivi karibuni, idadi ya wajumbe wa nyumba kumi iliongezwa kutoka 10 hadi 20, baada ya mabadiliko madogo ya Katiba ya CCM, lengo likiwa ni kuongeza ushiriki mpana wa wananchi na kupunguza mianya ya vitendo vya rushwa.
Katika uchaguzi huu, CCM imesisitiza haitawabeba wagombea kama ilivyokuwa mwaka 2020. Badala yake, chama kimedhamiria kumteua mgombea kwa kuzingatia kiwango chake cha kukubalika kwa wananchi wengi, ili kupunguza changamoto ya kuwaeleza na kuwashawishi wananchi kuhusu wagombea wakati wa kampeni.Lakini baadhi ya wachambuzi wa siasa wanasema, kujitokeza kwa watiania wapya imekuwa changamoto mpya kwa wabunge waliopo madarakani.
Wanaingia kwenye kinyang’anyiro wakiwa na fikra mpya na maono mapya ya kuleta maendeleo kwenye majimbo wanayotaka kugombea.
Na wengi wao wanachambua kwa makini upungufu wabunge waliopo madarakani, jambo ambalo linaleta changamoto kubwa kwao.