
Mbeya. Idadi ya vifo vilivyotokana na ajali ya barabarani ikihusisha basi kampuni ya CRN na gari la Serikali vimefikia vinne.
Ajali hiyo ilitokea jana Jumanne, Februari 25, 2025 eneo la Shamwengo wilayani Mbeya ambapo basi hilo lilikuwa likilipita gari la Serikali na kusababisha vifo vya watu watatu papo hapo na majeruhi saba.
Waliofariki dunia papo hapo ni mwandishi wa habari wa kujitegemea, Furaha Simchimba, Daniel Mselewa ambaye ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya na utingo wa basi ambaye jina lake bado halijajulikana.
Ajali hiyo ilitokea wakati msafara wa CCM, mkoani Mbeya ukitoka kumsindikiza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Taifa, Fadhil Rajabu.
Leo Jumatano, Februari 26, 2025, taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kupitia Katibu Tawala, Rodrick Mpogolo, imeeleza kufariki dunia kwa aliyekuwa dereva wa ofisi hiyo, Thadei Focus.
Focus alikuwa miongoni mwa majeruhi saba waliokuwa wakipatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
Miongoni mwa majeruhi ni waandishi Epimarcus Apolnali (Chanel Ten), Seleman Ndelage (Dream FM) na Denis George ambaye ni mwandishi wa kujitegemea.
Endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi