Mwanza. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amemjibu Dk Godfrey Malisa aliyepinga uamuzi wa Mkutano Mkuu wa chama hicho kumpitisha mgombea urais, Samia Suluhu Hassan akieleza ulikiuka katiba ya chama hicho tawala huku ikiwa imepita siku moja tangu avuliwe uanachama.
Dk Malisa amefukuzwa uanachama Februari 10, 2025 baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro kuamua na kutangazwa na Katibu wake, Mercy Mollel.
Akizungumza leo Jumanne Februari 11, 2025 kwenye mkutano na wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi wa Mkoa wa Mwanza, Wasira amesema amegundua ana akili za kuhama hama baada ya kuhama vyama kadhaa vya kisiasa hapa nchini.
Amesema Katiba ya CCM haijavunjwa, kwa sababu imetengenezwa na mkutano mkuu na wenyewe ndiyo una mamlaka ya kubadili au kufuta kitu kwa sababu ndiyo unawakilisha wanachama wa chama hicho kikongwe nchini.
“Mwingine anasema ooh mmevunja katiba, tumevunjwa katiba gani? Katiba inatengenezwa na mkutano mkuu na mkutano mkuu una mamlaka ya kubadili, yakufuta maana mkutano mkuu ndio una wawakilishi wa wanachama wa chama chetu,” amesema na kuongeza;
“Lakini siwezi kumsema sana maana aliyesema maneno hayo nimegundua kumbe alikuwa NLD zamani akahama akaenda NCCR akahama, amehama sana kwa hiyo ana akili za kuhama hama,”amesema Wasira.

Wasira ameyasema hayo alipokuwa akizungumzia miradi iliyoachwa na Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli ilivyokamilishwa na kuendelea kutekelezwa na Serikali ya awamu ya sita kwa miaka minne ambayo amesema baadhi iliachwa chini ya asilimia 30, ukiwamo wa Bwawa la Kufua umeme kwa maji la Julius Nyerere, daraja la Kigongo-Busisi (JPM) na reli ya SGR.
“Sasa baada ya kusikia mambo mazuri hayo ya Tanzania nzima ya miradi mikubwa ya mkakati…mkutano mkuu ukasema linalowezekana leo lisingoje kesho, kwa hiyo mkutano mkuu ukaamua katika uchaguzi mkuu ujao ambao ni wa mwaka huu, Rais Samia awe mgombea wa chama chetu,”amesema kada huyo wa CCM.
Hata hivyo, mapema leo, Dk Malisa amezungumza na Mwananchi na ameendelea kusisitiza kuna utaratibu wa wazi wa wagombea wa nafasi ya urais wanavyopatikana, huku akisistiza utaratibu uliofanyika hivi karibuni wa kumpitisha Rais Samia kugombea nafasi hiyo haukuwahi kushuhudiwa ndani ya CCM.
Azimio la Rais Samia kuwa mgombea kwenye nafasi ya urais lilipitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM ambao ndiyo chombo cha mwisho cha uteuzi wa mgombea wa kiti cha urais kupitia chama hicho.
Itakumbukwa jana Februari 11, 2025, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel alitangaza kuvuliwa uanachama wa CCM kwa kada huyo.

Mchungaji Godfrey Malisa aliyefukuzwa CCM.
Mollel akizungumza mbele ya wandishi wa habari mjini Moshi jana alisema; “tulikuwa na kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro ambacho pamoja na mambo mengine kimemfukuza mwanachama wa CCM Dk Godfrey Malisa kwa sababu amekuwa akibeza uamuzi uliofanyika na Mkutano Mkuu CCM Dodoma Januari 19, 2025. Baada ya mkutano ule, Dk Malisa amekuwa akitoa matamko ambayo hayaleti umoja na mshikamano ndani ya chama na katika nchi yetu.”
Kifungu kilichotumika kumfukuza uanachama Dk Malisa, katibu huyo amekinukuu kuwa ni cha tatu(c) cha Katiba ya CCM.
Akitangaza uamuzi huo, Katibu Mollel alinukuu kifungu hicho kinachosema; ‘Mwanachama yeyote atakayekataa kumuunga mkono mgombea wa CCM aliyeteuliwa na kikao halali cha chama na kuthubutu kufanya kampeni za siri au wazi kumhujumu, atakuwa ametenda kosa la usaliti na adhabu ni kufukuzwa uanachama.’
Lakini uamuzi huo unapingwa na Dk Malisa ambaye ameiambia Mwananchi leo Jumaane kwamba hakushirikishwa na hakupewa barua yoyote ya kufukuzwa uanachama.
Lakini Mwananchi limemrejea Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mollel ili azungumzie madai ya Dk Malisa kuwa yatajibiwa na Diwani wa Kata ya Miembeni na Katibu Mwenezi mstaafu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Mohamed Mushi.

Mwananchi limebisha hodi kwa Mushi ili kupata undani wa sakata hili na akijibu kwa simu, amesema walimshirikisha Dk Malisa hatua anazochuliwa na aliitwa kujieleza kuanzia ngazi ya tawi hadi kata.
“Tulimtumia wito wa kuhudhuria kikao cha kamati ya maadili ya tawi Januari 26 na Januari 28, 2025, kun wazee wa chama tuliwatuma mpaka nyumbani kwake akasema atakuja na Januari 31,2025 alifika na kusomewa tuhuma zake na kutakiwa kujibu na alikiri video ile ni yake.
“Alipewa nafasi ya kusikilizwa ngazi ya tawi kwa kamati ya maadili ya tawi lakini hakuwa tayari kuzungumza, tukachukua hatua, maamuzi yakaenda hadi juu akafukuzwa uanachama, wenye mamlaka ya chama ni viongozi wa chama, jambo linaloamuliwa na kikao taarifa inaweza kutoka kwa barua au kwa mdomo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti Wasira amewashukuru wajumbe saba waliompigia kura za hapana katika mkutano mkuu huo akisema wamewakilisha mawazo tofauti ambayo hata manabii wa Mungu walikutana nayo.
“Watu saba wakasema hapana nikawashukuru sana mimi ni binadamu, kama Yesu Kristo alipigwa mijeredi na Wayahudi wenzake na Mtume Muhammad (S.W.W) alifukuzwa Makkah kwenda Madina sembuse mie ni nani, watu saba tu walitosha kuwakilisha wenye mawazo tofauti lakini maelfu wakasema ndiyo,” amesema Wasira.
Mkutano Mkuu wa chama hicho Taifa uliofanyika Januari 19, 2025, pamoja na mambo mengine, ulipitisha jina la mgombea urais CCM pamoja na kumchagua Wasira kama Makamu Mwenyekiti wa chama hicho.
Awali, Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula ameeleza katika miaka minne jimbo lake limepokea zaidi ya Sh400 bilioni kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye sekta ya usafirishaji, Afya, Elimu na Maji.
Naye Mbunge wa Ilemela, Dk Angelina Mabula amewaambia wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi kuwa Serikali imeanza kushughulikia fidia ya wananchi waliopisha ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza na fidia za ardhi zilizotwaliwa miaka ya nyuma.
Kabla ya uamuzi huo, wakazi wa Kata ya Shibula walikuwa na mgogoro wa ardhi kati yao na uwanja huo uliodumu kwa zaidi ya miaka saba tangu mwaka 2017.
Hata hivyo, mwaka 2024, Serikali iliumaliza mgogoro huo kwa kukubali kuwalipa fidia baada ya tathmini.
“Serikali inazifanyia kazi changamoto hizo, wakati wowote mtaanza kulipwa fidia zenu,” amesema Dk Mabula.