VIDEO: Simba yazuiwa kufanya mazoezi kwa Mkapa usiku, waitana kikao

Dar es Salaam. Uongozi wa Simba umeitisha kikao cha dharura usiku huu kujadili kuzuiliwa kwa timu yao kufanya mazoezi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam leo.

Simba ilienda uwanjani hapo saa 1:00 usiku muda ambao mchezo huo utachezwa kwa ajili ya kufanya mazoezini, lakini ilizuiwa na wanaosemekana kuwa makomandoo wa Yanga na hivyo kulazimika kuondoka.

 Habari za uhakika zimefichua, baada ya tukio hilo, Simba wameitisha kikao na muda mfupi ujao watatoa taarifa rasmi ya kile walichokiamua.

 “Tunakutana na kuna uamuzi mzito na mgumu ambao tunaweza kuuchukua ili iwe fundisho kwa mamlaka za soka juu ya kuheshimu kanuni,” kimesema chanzo cha uhakika kutoka Simba.

 Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally amesema watatoa taarifa rasmi. “Wakubwa wanajadiliana na punde watatoa tamko,” amesema Ahmed Ally.

Simba yazuiwa kufanya mazoezi kwa Mkapa usiku, waitana kikao

 Kwa mujibu wa kanuni ya 45 ya uendeshaji wa Ligi Kuu toleo la 2024, timu mgeni wa mchezo inaruhusiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja ambao utatumika kuchezwa mchezo husika kwa muda ambao mechi husika itaanza.

“Timu ngeni itafanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi angalau mara moja kabla ya siku ya mechi katika muda tarajiwa wa mchezo husika. Sababu zozote za kukwamisha timu mgeni kukidhi ipasavyo au kupata haki hii zitathibitishwa kwanza na Kamishna wa mchezo,” inafafanua kanuni hiyo.

Mkuu wa usalama viwanjani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambaye anasimamia usalama  wa mchezo huo wa kesho, ASP Hashim Abdallah akizungumzia tukio hilo amesema, ”Mpaka siwezi kutoa kauli yoyote , tukio ni kama linavyojieleza tutalitolea taarifa kwa viongozi wangu na wao ndio watatoa tamko juu ya hiki kilichotokea.”