VIDEO: Simba yamaliza kikao na Waziri Kabudi, Mangungu aikana Yanga

Simba nao wamemaliza kikao chao na Wizara ya Utamaduni, Sanaaa na Michezo huku ikikana ajenda ya mchezo dhidi ya Yanga kuzungumzwa kwenye mkutano huo.

Simba iliingia kwenye mkutano huo saa 9:23 alasiri, msafara wao ukatoka saa 11:33 jioni ambapo viongozi wake wakakutana kwa kikao kifupi wakiwa wamesimama kabla ya mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu kuzungumza na waandishi wa habari.

Wakati Mangungu anatoka, amesema kikao chao na Waziri Profesa Palamagamba Kabudi kimekuwa na ajenda ya maendeleo ya soka nchini.

Mangungu amesema kwa kuwa mkutano huo umekuwa wa makundi tofauti, inawezekana serikali imetofautisha ajenda za kikao hicho ambapo klabu yake haikujadili mchezo namba 184 wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Simba ambao uliahirishwa Machi 8, 2025.

“Tunashukuru kwamba tumezungumza yote ambayo yalikuwa ni ya umuhimu, tumeyawasilisha kwa mheshimiwa waziri na timu yake lakini vikao vitaendelea,” amesema Mangungu huku akiongeza.

“Tumejadili maendeleo ya soka Tanzania, maendeleo ya soka yako mengi, kuna maeneo ambayo kama mnavyofahamu Waziri ni mpya katika wizara hii pamoja na uzoefu mkubwa alionao nadhani kuna mambo yalitakiwa tujadiliane kwa pamoja.

“Kwanza hata sijui kama Yanga walifika hapa, leo tumeanza kikao cha awali lakini kuna vikao vitaendelea, kikao chetu sisi hakihusiani na chao (Yanga) kama kingehusiana na chao nadhani tungekaa pamoja, wao walipokutana na waziri wanajua walichozungumza naye na kama walijadili hilo ni sawa lakini sisi haya ninayoyaeleza ndio tuliyojadili.”

Akijibu kuhusu hatma ya mchezo wa Kariakoo Dabi, Mangungu amesema: “Mamlaka si ilishasema mechi itapangiwa tarehe, kuna haja gani tena ya kusema hatma yake, mechi itachezwa siku nyingine kama itakavyopangwa, wao wameshikilia kanuni lakini kanuni hiyohiyo inaipa Bodi ya Ligi kuahirisha mechi pale inapoona inafaa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *