Dar es Salaam. Waombolezaji wameungana na familia kuupokea mwili wa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru uliowasili leo Jumanne Novemba 12, 2024 Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mwili wa Mafuru umewasili saa 7:45 mchana kutokea India na saa 10:15 msafara wa magari zaidi ya 50 ulianza kuelekea Hospitali ya Lugalo kwa ajili ya kuuhifadhi.
Tukio la kupokea mwili huo liliongozwa na baba wa marehemu aliyekwenda kuutambua mwili wa kijana wake kabla ya kutoka nje ya uwanja.
Mafuru aliyekuwa mtaalamu wa fedha na uchumi nchini Tanzania akihudumu katika sekta binafsi na ya umma, alifariki dunia Jumamosi, Novemba 9, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Apollo nchini India.
Zitto afunguka
Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema ilimchukua muda kuamini Lawrence Mafuru amefariki dunia, kwa kuwa ni mtu wa rika yake aliyemtegemea katika kuimarisha nchi.
Zitto amesema hayo leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa ni miongoni mwa waombolezaji waliojitokeza kupokea mwili wa Mafuru.
Endelea kufuatilia Mwananchi.