Dar es Salaam. Mwili wa kijana ambaye hajafahamika jina lake, umekutwa kando Barabara ya Mandela eneo la Tabata Relini jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo limetokea jana Jumatatu Setemba 22, 2024, saa nne mchana baada ya wenyeji wa eneo hilo kumtilia shaka wakidai wamemuona amelala kwa siku nne bila kuamka.
Akizungumza na Mwananchi eneo hilo, Zena Mohamed ambaye ni mamalishe amesema kijana huyo amelala eneo hilo linatumiwa na watu tofauti wanaojishughulisha na uokotaji wa makopo lakini walipata hofu baada ya kumuona haondoki.
“Huyu kijana leo (jana) ni siku ya nne tangu alale hapa, hivyo jana (juzi) tukamuona tena tukajiuliza mbona ageuki, kuna baba mmoja ni mlinzi shirikishi tukamfuta kumueleza kuna kijana ana siku ya tatu hageuki tunaomba ukamuangalie kama ni mzima au kafa tukaja naye hapa saa saba mchana,” amesema.
Amesema baada ya kufika huyo mzee aliwajibu anapumua kwa mbali, hivyo walitaka kujua kitu gani wanaweza kufanya kwa ajili ya kumsaidia ikiwamo kumpa chakula wakihofia atakuwa na njaa ndio sababu ya yeye kulala hapo.
Amesema kutokana na uoga wa kupewa kesi, waliogopa kumuhudumia hivyo walimuacha aendelee kulala eneo hilo na wao kuendelea na shughuli zao za kila siku.
“Leo (jana) dada yangu baada ya kuona bado amelala ikabidi ampigie simu mwenyekiti wa Serikali ya mtaa na alipofika hapa alipigia simu polisi,” amesema Zena.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabibo, Said Kitogo amesema alipigiwa simu na wananchi kuhusu tukio hilo, ndipo akatoa taarifa polisi ambao walifika na kuubeba mwili kuupeleka Hospitali ya Mwananyamala.
“Nimefika hapa baada ya kupigiwa simu na wananchi na kukuta mwili umelala hapa, nikiambiwa ni siku ya tatu hageuki na taarifa hizi nilizipata saa saba mchana,” amesema Kitogo.
Shuhuda wa tukio hilo, Amos Tamba ambaye ni dereva wa pikipiki Kituo cha Mwananchi amesema kijana huyo huwa anapita eneo hilo na kupumzika lakini hawajui anapoishi licha ya kuwa na utaratibu wa kupita mara kwa mara.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Zavery Benela amesema wamepokea mwili wa mwanamume kutoka Mabibo External.
“Kweli umepokewa mwili wa mwanamume lakini hajafahamika kutoka eneo la Mabibo External,” amesema Dk Benela.