Geita. Mvua iliyonyesha kwa saa mbili Mjini Geita imesababisha mafuriko ya baadhi ya maeneo kujaa maji, kuta za nyumba kuanguka na watu 15 kujeruhiwa huku wengine wakiwahishwa hospitali baada ya kunywa maji.
Kutokana na mvua hiyo iliyoanza kunyesha saa sita mchana wa leo Novemba 5,2024, baadhi ya makazi na maeneo ya biashara yamejaa maji huku miundombinu kama ya barabara nayo ikiharibiwa ikiwemo Kituo Kikuu cha Mabasi Geita.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Hamis Dawa amesema mvua hiyo imesababisha baadhi ya maeneo kujaa maji huku nyumba za maeneo ya Mtaa wa Mbugani zikizingirwa na maji.

Maji yakiwa yamejaa eneo la stend ndogo ya magari katika kituo kikuu cha mabasi mjini Geita
“Saa sita mvua ilinyesha tulipokea simu kuna maeneo yamezingirwa na maji Mtaa wa Mbugani tumeokoa watu watano, Mtaa wa Stendi maji yamejaa na watu watatu wameokolewa, Mbagala watoto wanne na huko Uwanja wa Nyankumbu watatu walizingirwa na maji,“ amesema Dawa.
Dawa amesema katika Mtaa wa Jimboni nyumba moja imeanguka ambapo wakazi wa nyumba hizo wamehamia kwa majirani.
Aidha amewataka wananchi hususan wanaoishi maeneo ya mabondeni kuchukua tahadhari ya kuhama kipindi hiki cha mvua.
Mashaka Lucas, Mkazi wa Geita amesema maji mengi yaliyojaa kituo cha mabasi yametokea maeneo ya mlimani huku eneo la mbugani likiathiriwa zaidi.
Marsela Slaus, mfanyabiashara eneo la stendi amesema kilichosababisha maji kujaa ni mitaro kuziba ambapo kutokana na hilo wamepata hasara ya bidhaa kuharibika na baadhi ya magari kuingia maji.

“Maji huwa yanajaa lakini yanatoka kwa haraka leo hali imekuwa tofauti walivyojenga eneo hili waliziba mitaro hivyo maji hayatoki ndio maana yamejaa.”
“Leo vitu vyetu vimeharibika tunaomba Serikali ione namna ya kutatua changamoto hii,” amesema Slaus.