Mbeya. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya imeahirisha shauri la kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdude Nyagali baada ya wajibu maombi kukosa kiapo kinzani na sasa itasikilizwa Alhamisi ya Novemba 28, 2024.
Kesi hiyo namba 33247/2024 iliyofunguliwa mahakamani hapo kupitia mawakili wa utetezi wakiongozwa na Boniface Mwabukusi na Philip Mwakilima kuiomba Mahakama iwaamuuru Kamanda wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi (RCO) mkoani Songwe kumfikisha mahakamani kada huyo iwapo ana kesi ya kujibu.
Pia, mawakili hao wanaomba kuachiwa huru Mdude iwapo hana hatia yoyote.
Mdude alikamatwa Novemba 22, 2024 akiwa na viongozi wengine wa Chadema akiwamo mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe na mwenyekiti wa Kanda ya Nyansa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu.
Siku moja baadaye wao waliachiwa huku kada huyo akibaki mikononi mwa polisi mkoani Songwe kwa ajili mahojiano.
Jana Jumatatu, Kamanda wa Polisi mkoani Songwe SACP, Agustino Senga akizungumza na Mwananchi alisema walikuwa wamemaliza kumhoji Mdude na alikuwa amepelekwa tena mikononi mwa jeshi hilo mkoani Mbeya kwa mahojiano mengine, kujibu tuhuma zinazomkabili.
Amesema Mdude alikuwa na kesi katika mambo matatu yaliyokuwa yanamkabili na kilichobaki ni mambo ya kitaalamu, hivyo kama itakuwa ni kupata dhamana itafahamika mkoani Mbeya.