VIDEO: Anayekumbatia njiti Hospitali ya Amana akabidhiwa nyumba

Dar es Salaam. Mama aliyejitolea kukumbatia watoto njiti katika Hospitali ya Rufaa Mkoa Amana, Mariam Mwakabungu (26) ameangua kilio baada ya kukabidhiwa nyumba ya makazi yenye thamani ya Sh45 milioni iliyopo Chanika – Zavara jijini Dar es Salaam.

Nyumba hiyo aliyozawadiwa na msamaria mwema (hajataka kutajwa jina) imejengwa na Taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kushirikiana na wadau wengine waliochangia baadhi ya vitu wakati wa ujenzi wake.

Pamoja na nyumba hiyo, Julai 20, 2023 Serikali kupitia Wizara ya Afya, ilitoa ajira ya mkataba kwa Mariam, ikiwa ni siku moja tangu Rais Samia Suluhu Hassan kutuma salamu za pongezi zilizoambatana na fedha taslimu Sh2 milioni.

Mwonekano wa nyumba mbele na nyuma.

Akikabidhiwa nyumba hiyo jana jioni Jumapili, Novemba 17, 2024 kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti Duniani, Mariam aliyefikishwa eneo hilo akiwa amefungwa kitambaa usoni, alianguka chini kwa mshangao na kulia kilio cha furaha akiwa na mume wake, Christopher Nyoni (30).

Mariam aliyeongozana na bibi yake aliyemlea, ametoa shukrani zake kwa msamaria mwema aliyechangia nyumba hiyo kujengwa na wadau wengine.

“Sijategemea kitu kama hiki, nawashukuru sana Mwenyezi Mungu awabariki. Pia, natoa shukurani zangu za dhati kwa Hospitali ya Amana kwa kuweza kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu wa kukumbatia watoto hawa kwa maana bila wao kunipa nafasi tusingekuwa hapa leo,” amesema Mariam.

Anayekumbatia watoto njiti alivyokabidhiwa nyumba ya kisasa

“Nawashukuru watumishi wote wa Amana kwa kunipa mafunzo ya namna ya kutoa huduma kwa watoto njiti na bado naendelea kujifunza. Navishukuru vyombo vya habari kwa kupeleka kwa jamii kile ninachokifanya,” amesema Mariam ambaye hapo awali alikuwa amepanga nyumba maeneo ya Tabata Kinyerezi.

Mwakilishi kutoka Doris Mollel Foundation, Dk Sylivia Ruambo amesema Mariam alianza kujitolea kukumbatia watoto hao ngozi kwa ngozi lakini upendo alioutoa umerudi kwake kwa msamaria mwema kuguswa na kumzawadia nyumba hiyo.

“Matendo mema siku zote yanazaa, matamanio ilikuwa kumpatia makazi baada yakumtembelea nyumbani kwake na kuona maisha anayoishi, DMF ilikutana na mtu mmoja kati ya wanaosaidia watoto njiti huyu mtu machozi yalimtoka kwa jinsi ambavyo Mariam amefanya, akatuagiza kuhakikisha Mariam anapata makazi.

“Akasema katafuteni kiwanja mkipata mtatuambia. Nilitafuta na tulipopata kililipiwa na akatoa fedha za awali ujenzi uanze,” amesema.

Mama aliyejitolea kukumbatia watoto njiti katika Hospitali ya Rufaa Mkoa Amana, Mariam Mwakabungu (26).

Dk Ruambo amesema nyumba hiyo ilianza kujengwa Desemba mwaka 2023 na imekamilika Novemba mwaka huu.

“Tunaadhimisha kwa kutambua mchango wa Mariam kwa kuhakikisha anapambania ajenda ya mtoto njiti. Yeye alifanya tukio la imani na jambo la kipekee.

Kupitia yeye tunatuma ujumbe kwa Serikali kuhakikisha huduma za watoto njiti zinaboreshwa na kunakuwa na kina Mariam wengine wengi ili kufikia ajenda ya Rais Samia Suluhu Hassan kupunguza vifo vya watoto hawa nchini,” amesema.

‘Karma imemfuata Mariam’

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Temeke, Dk Joseph Kimaro amesema karma imemfuata Mariam kwa kuwa jambo analolitenda kwa jamii linamrudia kwa nguvu kubwa.

“Katibu Mkuu ameniagiza anaishukuru Doris Mollel Foundation kwa kuokoa watoto wengi njiti ambao wangekuwa miongoni mwa waliofariki. Tuwajali watoto njiti na wenye uzito pungufu, mtoto ni wa jamii anaweza kulelewa na jamii akakua vema na mambo mengine yakaenda vizuri,” amesema.

Dk Kimaro amesema ilitarajiwa mtoto alelewe na mama yake, lakini kutokana na changamoto za vifo vya kinamama wasio na ndugu, watoto kutupwa na kinamama wanaojifungua na kulazimika kuwa katika matibabu wakishindwa kutunza watoto njiti, hilo linafanywa na mama wa kujitolea kama Mariam.

“Umejitoa kuiboresha huduma na kutusaidia kuiboresha, unadhani umefanya jambo dogo lakini umepunguza idadi ya watoto ambao wangefariki, umepunguza namba kwa Taifa ni kazi ambayo Rais Samia anaisimamia kwa nguvu, ameingia mikataba ya wakuu wa Mikoa katika utekelezaji wa kampeni ya ‘Pamoja Tuwavushe Salama,” amesema.

Katika hatua nyingine Dk Kimaro ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Amana kwa kuwa wakati wanaanza mchakato wa kuruhusu Mariam afanye hiyo kazi, hakukuwa na mwongozo wowote katika eneo hilo.

Ofisa Ustawi wa Jamii ambaye aliiwakilisha Hospitali ya Amana, Sufian Mndolwa amesema Amana ilitendewa jambo jema na Mariam jukumu lililokuwa la kwao, lakini alijitokeza akabeba jukumu hilo.

Amesema haikuwa rahisi katika siku za mwanzo Mariam anajitolea hospitalini hapo kwa maana ilitakiwa awe anapewa chakula na hospitali.

“Ustawi wa jamii tulikuwa tunatoa chakula kwa Mariam, siku moja ilifika jioni Mariam hajapelekewa chakula, nikawaomba manesi wachangishane apate kula ili aendelee na kazi ya kukumbatia watoto alifanya kwenye mazingira haya mwanzo.

“Tulimkaribisha Mariam kwa sababu wamama walikuwa wanazaa watoto na wanatekeleza, mtoto anahitaji joto si hili tunaloliona Mariam akaamua kupambana ilhali wanawake wenzake waliamua kuwaacha.

“Mmoja alitelekeza mtoto tukaamua kumtafuta na kumkabidhi alienda akamuacha Buguruni Chama, wale watoto ambao walikuwa Mariam anawakangaroo Amana wapo hatua za mwisho kuchukuliwa na wazazi wa kuasili wakalelewe katika maisha wanayoyahitaji,” amesema Mndolwa.