Mwanza. Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Dell Simancas amerekodi tukio la mwanaye, Adrian Simancas (24) akimezwa na samaki aina ya Nyangumi mwenye nundu kisha kumtapikwa akiwa hai.
CNN imeripoti kuwa tukio hilo la kushtua limetokea Jumamosi Februari 8, 2025, wakati Adrian na baba yake walipokuwa wakipiga kasia kila mmoja kwenye boti yake inachoelea majini (Kayaker) katika Bahari ya Kusini mwa Mkoa wa Patagonia nchini Chile.
Jambo la kushangaza, wakati tukio hilo linatokea, baba mzazi wa Adrian alijiongeza na kuanza kurekodi video kwa kile alichodai kuwa alishawishika kufanya hivyo baada ya kuanza kuona mawimbi makubwa yanayovutia.
Kipande cha video kilichowekwa mtandaoni kinamuonyesha, nyangumi huyo akiinuka kutoka kina kirefu cha maji kisha kummeza, Adrian na kutoweka naye.
Katika video hiyo, iliyothibitishwa na CNN, Dell ambaye ni baba yake Adrian, anasikika akimuita mwanawe ambaye alikuwa ametapikwa na nyangumi, akimwambia “shika boti.”
Kisha Adrian aliogelea kuelekea kwenye boti ya baba yake na kuishikilia huku wakijaribu kukimbia eneo hilo.
“Nadhani amenimeza,” Adrian amesikika akizungumza kwenye video hiyo.
Akizungumza na CNN en Español, Adrian ameeleza jinsi ilivyohisi kuwa ndani ya nyangumi huyo mwenye nundu kwa muda mfupi.
“Nilipogeuka nilihisi kitu kama ute ute usoni mwangu; niliona rangi kama bluu iliyokolea, nyeupe, kitu fulani kilichokuwa kinanijia kutoka nyuma na kisha kikafunga… na kunizamisha,” anasema Adrian.
“Wakati huo, nilifikiria kuwa hakuna kitu kingine ningeweza kufanya, nilihisi nitakufa, sikujua ni nini kilichokuwa kinatokea.”
Lakini licha ya hofu hiyo, alihisi jaketi okozi alilokuwa amevaa wakati wa kupiga kasia katika bahari hiyo ndilo lililosababisha kuelea kwa urahisi baada ya kutapikwa na nyangumi huyo. Kwa mujibu wa Adrian alijikuta juu ya uso wa maji tena na ndipo alipoanza kuelewa kilichotokea.

Dell ameiambia CNN en Español kwamba, baada ya kuona mawimbi ya kuvutia na kuanza kurekodi, anasema: “Nilisikia kama wimbi kali likipiga nyuma yangu, nilipogeuka sikumuona, Adrian wala boti yake hivyo nikaanza kuwa na wasiwasi. Baada ya kama sekunde tatu, nilimuona akijitokeza juu ya maji.”
Walipoulizwa kama wangerejea kuendesha boti hizo (Kayaker), wote wawili walijibu kwa pamoja: “Bila shaka.”
Hata hivyo, mtaalamu wa wanyama, Vanessa Pirotta amesema mpigakasia huyo huenda alijikuta mdomoni mwa nyangumi huyo wakati alipokuwa akila viumbe maji ama samaki kwa njia inayofahamika kama “lunge-feeding’.
“Mtu huyo alijikuta karibu sana na nyangumi aliyekuwa akila. Hakuingizwa ndani kabisa.
“Viumbe hawa hawalengi mawindo yenye ukubwa wa binadamu. Hawana uwezo mkubwa wa kummeza binadamu,” amesema Vanessa, akieleza kuhusu koo la nyangumi kuwa ni jembamba na pia hawana meno.
Mlango Bahari wa Magellan ni eneo maarufu la utalii kutokana na shughuli zake za nje na uwepo wanyamapori hususan ni nyangumi na papa.
Miongoni mwa shughuli zinazotajwa kuwepo katika mlango bahari huo ni pamoja na utalii wa kupiga kasia (Kayaker), utalii wa nyangumi na pomboo.
Nyangumi wenye nundu wanaishi katika bahari kubwa duniani kote, kulingana na maelezo ya Mamlaka ya Kitaifa ya Bahari na Anga (NOAA).
NOAA inasema nyangumi wenye nundu ni maarufu kwa watalii wanaofika kuwatazama kwa sababu mara nyingi huonekana wakiruka juu ya maji na kupiga maji kwa mapezi yao marefu ama mikia yao.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.