Viboko hadi kifo vikomeshwe shuleni

Matukio ya hivi karibuni ya vifo vya wanafunzi kutokana na adhabu ya viboko yanashtua na kuibua mjadala mzito kuhusu nidhamu na haki za watoto wawapo shuleni.

Kumekuwa na taarifa za matukio mengi ya walimu kuwaadhibu isivyo wanafunzi kwa viboko, kiasi cha kusababisha maumivu makali, majeraha, ulemavu na hata kifo.

Adhabu hizi zimekuwa zikitolewa na walimu bila kuzingatia miongozo ya kanuni na sheria za utoaji adhabu dhidi ya makosa mbalimbali zilizowekwa na Serikali kwa mujibu wa sheria na hivyo kusababisha madhara makubwa si tu kwa watoto pekee bali wazazi na uongozi wa shule kwa jumla.

Vifo vya karibuni vya Mhoja Maduhu, mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari Mwasamba na Jonathan Makanyaga, mwanafunzi wa darasa la kwanza mkoani Kilimanjaro, ni ushahidi wa ukatili huo unaofanywa na baadhi ya walimu kwa kisingizio cha nidhamu.

Sheria za utoaji wa adhabu ya viboko zipo, lakini bado hazizingatiwi. Kanuni ya mwaka 2002 9G.N.294) inaagiza viboko visizidi vinne na vinapaswa kutolewa tu kwa makosa makubwa, kwa idhini ya mwalimu mkuu na kuandikwa kwenye rejista.

Lakini, matukio haya yanaonyesha kwamba baadhi ya walimu wamejigeuza wanyanyasaji, wakitoa adhabu kali hadi kuua. Ni wazi kuwa mfumo wa utoaji adhabu unahitaji marekebisho makubwa na udhibiti madhubuti.

Hakuna kinachoweza kuhalalisha mwalimu kumpiga mwanafunzi kwa hasira, hadi kumsababishia majeraha makubwa au kifo. Jamii inapaswa kutafakari, je, lengo la elimu ni kuwajenga watoto kiakili na kitabia au ni kuwanyanyasa na kuwatengenezea hofu isiyo na msingi?

Tunafahamu kuwa walimu hufundishwa kwenye saikolohjia kwamba kumpiga mtoto kwa hasira kunaweza kumsababishia hofu, wasiwasi, na kupunguza kujiamini.
Pia, anaweza kujenga chuki, kisasi au hali ya kujiona hana thamani. Pia, huathiri uwezo wake wa kujifunza na kuathiri mahusiano yake na walimu au wazazi. Matokeo yake, mtoto anaweza kuwa mkimya kupita kiasi, muoga au hata kuwa na tabia za ukaidi na jeuri.

Taifa linapaswa kuepukana na masuala hayo ingawa si lazima kufuata mifano ya nchi zilizoendelea ambazo zimepiga marufuku kabisa viboko shuleni na zimefanikiwa kujenga nidhamu kupitia mbinu za malezi chanya.

Serikali inapaswa kuchukua hatua kali kwa wote wanaovunja sheria kwa kutumia viboko visivyo halali. Vyombo vya usimamizi wa elimu vinapaswa kuhakikisha kuwa walimu wote wanapata mafunzo ya mbinu mbadala za nidhamu zinazomlinda mtoto.
Aidha, vyombo vya sheria vinapaswa kuchunguza matukio haya kwa kina na kuwachukulia hatua kali wahusika, ili iwe fundisho kwa wengine.

Pia, wazazi wanapaswa kushirikishwa katika malezi na nidhamu ya watoto wao shuleni. Kabla ya adhabu yoyote, ni muhimu mtoto apewe nafasi ya kujieleza, na inapowezekana mzazi wake ahusishwe.

Nidhamu ya mtoto haipaswi kuwa jukumu la mwalimu pekee bali ni jukumu la pamoja kati ya shule, mzazi, na jamii nzima.

Tunapopoteza watoto kwa sababu ya viboko shuleni, tunapoteza kizazi cha kesho. Lazima kama jamii tuseme “hapana” kwa aina hii ya ukatili.

Serikali na wadau wa elimu wanapaswa kuchukua hatua madhubuti sasa, kabla hatujashuhudia maafa zaidi. Viboko visivyofuata sheria lazima vikome mara moja.