
Arusha. Wimbi la uhalifu, hususan linalotekelezwa na makundi ya vijana wa mitaani maarufu kama vibaka, limeendelea kuwa tishio katika Jiji la Arusha, ambapo tukio la hivi karibuni limemgusa mtu aliyedaiwa kutambuliwa kuwa dereva wa lori, Maulid Rajabu (35), kudaiwa kuuawa kwa kuchomwa visu na kisha kutupwa pembezoni mwa barabara na watu wanaodaiwa kuwa vibaka.
Mauaji hayo yametokea wakati ripoti ya Hali ya Uhalifu iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, ikionyesha kuwa Jiji la Arusha linashika nafasi ya nne kitaifa kwa kuwa na matukio 699 ya uhalifu.
Matukio hayo yanajumuisha mauaji, ubakaji, pamoja na ukwepaji wa majukumu ya malezi ya watoto.
Tukio la mauaji ya dereva Maulid Rajabu limetokea Alhamisi, Mei 15, 2025, majira ya saa 1:00 usiku katika Mtaa wa Longdong, Jiji la Arusha, wakati Rajabu kabla ya kukutwa na umauti alipokuwa akitafuta nyumba ya kulala wageni baada ya kurejea kutoka safarini.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, hajapatikana ili kutoa ufafanuzi kuhusu tukio hilo, licha ya juhudi za kumpata kufanywa.
Balozi wa Shina Namba Tatu katika Mtaa wa Longdong, Ramadhani Mbaga amethibitisha kutokea tukio hilo, akieleza kuwa aliwasili katika eneo la tukio baada ya kupokea taarifa kutoka kwa msamaria mwema.
“Nilipokea taarifa kuwa kuna mwili umeonekana pembezoni mwa barabara. Nilipofika eneo la tukio nilikuta mwili ukiwa umefunikwa, ukiwa na majeraha makubwa sehemu ya mbavu na kifuani.
“Tulitoa taarifa kwa polisi, ambao walifika na kuuchukua mwili kisha kuupeleka kuhifadhiwa katika Hospitali ya Mount Meru,” amesema Mbaga.
Akielezea walivyomtambua marehemu, Mbaga amesema kuwa wamefanikiwa kujua majina yake baada ya kutambuliwa na mmoja wa wakazi wa eneo hilo.
“Huyu mtu sio mkazi wa eneo hili lakini katika upelelezi wa Jeshi la Polisi tulifanikiwa kupata mkazi mmoja wa mtaa huu ambaye amemfahamu kwa majina na mkazi wa Mlangarini,” amesema Mbaga.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Longdong, Gerald Saitoti amesema hali ya usalama kwa sasa inahitaji juhudi za pamoja katika kudhibiti makundi ya vijana wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.
“Makundi haya ya vijana wanatumia bodaboda kama njia ya kutekeleza uhalifu, jambo linaloongeza changamoto kubwa katika kuwabaini na kuwakamata.
“Vijana hawa hutekeleza uhalifu wakiwa kwenye makundi ya zaidi ya wawili, na mara nyingi wanakuwa na silaha kama mapanga na visu. Tunahitaji nguvu za ziada ili kuweza kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria. Ingawa baadhi yao wamekamatwa, mara nyingi huachiliwa na kurejea mitaani,” ameongeza.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti kuhusu tukio hilo, Rebeka Halfani alieleza kuwa saa saba usiku, Maulid Rajabu alifika Miami Rest House kutafuta chumba cha malazi. Hata hivyo, hakuridhika na chumba alichokiona na aliamua kutafuta mahali pengine.
“Walikuja wanaume wawili, akiwemo Rajabu, ambaye baada ya kuangalia chumba hakuridhika nacho, hivyo nikamfungulia geti akienda kutafuta sehemu nyingine,” alisema Rebeka, na kuongeza: “Asubuhi, tulipokea taarifa kuwa mtu amekutwa ameuawa na mwili wake kutupwa kando ya barabara. Nilipokwenda kuona nilikumbuka ni yeye aliyekuwa kwangu kutafuta chumba usiku.”
Mohamed Mussa ameeleza kuwa matukio ya uporaji na raia kujeruhiwa katika mitaa ya Jiji la Arusha yamekuwa ni kero kubwa na tishio kwa usalama wa wananchi.
Ameomba Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka ili kudhibiti matukio hayo, akisema kuwa baadhi ya wahalifu wanapokamatwa, huachiwa na kurejea mitaani.
“Kila mwezi tunachangia Sh1,000 kwa kichwa kuwalipa Sungusungu (Ulinzi Shirikishi mitaani), lakini hakuna mabadiliko, kwani uhalifu umeendelea na mbaya zaidi, wanasababisha mauaji,” amesema Mussa.