Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela amepongeza misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kukabiliana na uingiliaji kati wa serikali ya Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela.
Yvan Gil, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela ametuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram akishukuru misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mkabala wa uingiliaji kati wa hivi karibuni wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela.

Gil ameandika kuwa: Uingiliaji kati wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela ni kukariri stratejia zilizofeli huko nyuma za nchi hiyo.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela amesisitiza udharura wa kuendelezwa umoja kati ya Caracas na Tehran na kuongeza kuwa, Iran na Venezuela, kwa kushikamana pamoja, zitaendeleza mapambano ili kuwa na dunia yenye amani na uadilifu.
Wananchi wa Venezuela walimchagua Nicolás Maduro katika uchaguzi wa rais uliofanyika Julai 28 mwaka huu. Hata hivyo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Anthony Blinken, alidai kuwa Edmundo González, mwanadiplomasia wa zamani na aliyeko uhamishoni, ndiye rais aliyechaguliwa wa watu wa Venezuela.
Ismail Baqae Hamaneh Msemaji wa Wizara ya Mambo ya NJe ya Iran amelaani uingiliaji kati wa Marekani na baadhi ya waitifaki wa nchi hiyo katika masuala ya ndani ya Venezuela na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inauhesabu uingiliaji kati wowote wa nchi ajinabi katika masuala ya ndani ya Venezuela kuwa ni kinyume cha sheria za kimataifa na kanuni za Hati ya Umoja wa Mataifa; na inaamini hatua hiyo itavuruga amani na utulivu wa Venezuela.