Vatican: Makadinali wanaopewa nafasi kubwa kumrithi Papa Francis

Makadinali wa Kanisa Katoliki duniani, kuanzia siku ya Jumatano Mei 7, watakutana Vatican, kumchagua Papa mpya, baada ya kifo cha Papa Francis mwezi Aprili.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 3

Matangazo ya kibiashara

Wakati wa uchaguzi huo, Makadinali 133 walio chini ya umri wa miaka 80, watashiriki kwenye zoezi la kumpata kiongozi mpya wa Kanisa hilo duniani lenye waumini zaidi ya Bilioni 1.2.

Siku ya Jumatano, mchakato huo wenye usiri mkubwa, utaanza na kipindi cha maombi kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.

Kuelekea uchaguzi huo, hakuna kampeni rasmi, wala orodha ya wale wanaowania kuwa Papa. Hata hivyo, kuna Makadinali 15 wanaopewa nafasi kubwa ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo.

KUTOKA BARANI ULAYA

Pietro Parolin, alipokutana na rais Emmanuel Macron, mjini Vatican
Pietro Parolin, alipokutana na rais Emmanuel Macron, mjini Vatican AFP – SIMONE RISOLUTI

Pietro Parolin raia wa Italia mwenye umri wa miaka, 70. Wakati wa uongozi wa Papa Francis, alikuwa Mkuu wa shughuli za Vatican. Wanaomfahamu, wanamwelezea kama mtu mtulivu, mpole na mchangamfu.

Pierbattista Pizzaballa (Italia), mwenye umri wa miaka 60. Ni mwakilishi mkuu wa Kanisa Katoliki katika eneo la Mashariki ya Kati, akihudumu katika Makanisa ya Jordan, Israeli, Palestina na Cyprus.

Matteo Maria Zuppi (Italia), 69, Askofu Mkuu wa Bologna. Amewahi pia mwanadiplomasia wa Vatican, kwa miaka 30, akiwa mjumbe maalum nchini Ukraine.

Claudio Gugerotti (Italia), 69, mtaalam wa madhehebu ya Makanisa ya Mashariki. Amewahi pia Balozi wa Vatican, nchini Georgia, Armenia, Azerbaijan, na baadaye Belarus. Kati ya mwaka 2015-2020 alihudumu nchini Ukraine.

Makadinali wengine kutoka Ulaya, wanaopewa nafasi ya kuchaguliwa ni pamoja na Jean-Marc Aveline (Ufaransa), 66, Askofu Mkuu wa Marseille, Anders Arborelius (Sweden), 75, Askofu wa Stockholm, Mario Grech (Malta), 68, Askofu mstaafu wa  Gozo, Peter Erdo (Hungary), 72, Askofu Mkuu-Budapest, Jean-Claude Hollerich, 66, Askofu Mkuu wa Luxembourg.

KUTOKA BARANI ASIA

Kadinali Luis Antonio Gokim Tagle
Kadinali Luis Antonio Gokim Tagle © AFP – TIZIANA FABI

Kadinali Luis Antonio Tagle (Ufilipino), 67, Askofu Mkuu mstaafu wa Manila. Tagle, mwenye sifa ya uchangamfu, mtumiaji mkubwa wa mitandao ya kijamii. Anafahamika kwa kulikosoa Kanisa na kuwa karibu na watu wenye maisha ya chini. Mwingine ni Charles Maung Bo (Myanmar), 76, Askofu Mkuu wa jimbo kuu la Yangon

KUTOKA BARANI AFRIKA

Peter Turkson (Ghana), 76,  Askofu Mstaafu wa jimbo kuu la  Cape Coast. Mmoja wa Makadinali wenye ushawishi mkubwa kutika barani Afrika. Amekuwa akitajwa kuwa huenda akawa, Papa wa kwanza Mwafrika. Aidha, aliwahi kuwa mpatanishi wa Vatican, kuhusu mzozo wa Sudan Kusini. Msimamo wake ni kuwa mapenzi ya jinsia moja sio haki za binadamu, licha ya kupinga unyanyasaji wa mashoga.

Robert Sarah (Guinea), 79. Anafahamika kwa sifa yake ya kuhifadhi mapokea asili ya Kanisa Katoliki. Mpinzani wa mapenzi ya jinsia moja na utoaji mimba. Wachambuzi wanasema, kutokana na msimamo yake mikali, ni vigumu kuchaguliwa kuwa Papa.

Fridolin Ambongo Besungu (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), 65, Askofu Mkuu wa Kinshasa. Amekuwa katika mstari wa mbele, kupigania amani katika nchi yake. Anapinga Kanisa Katoliki, kuwabariki wapenzi wa jinsia moja. Ambongo, mwaka 2013 alisema, sura ya Kanisa Katoliki duniani, ni Afrika.

Kadinali Fridolin Ambongo.
Kadinali Fridolin Ambongo. © Gregorio Borgia / AP

KUTOKA BARANI AMERIKA

Robert Francis Prevost (Marekani ), 69, Askofu Mkuu mstaafu wa jimbo kuu la  Chiclayo. Tangu mwaka 2023 amekuwa akimshauri Papa kuhusu uteuzi wa Maaskofu wapya.

Timothy Dolan (Marekani), 75, Askofu Mkuu wa jimbo la New York. Mtaalam wa masuala ya theolojia, mpinzani mkubwa wa utoaji mimba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *