Van Nistelrooy uso kwa uso na Amorim

Manchester, England. Aliyewahi kuwa kocha wa msaidizi wa Manchester United, Ruud Van Nistelrooy ataiongoza Leicester City leo saa 5:00 usiku katika mchezo wa Kombe la FA utakaochezwa kwenye uwanja wa Old Trafford dhidi ya Manchester United ambayo kwa sasa inaongozwa na Ruben Amorim.

Imepita miezi minne tangu Van Nistelrooy kuondolewa United baada ya ujio wa Amorim ambaye aliweka wazi kuwa hayupo tayari kufanya kazi na kocha huyo.

Kabla ya kuondoka United, Van Nistelrooy aliiongoza timu hiyo kama kocha wa muda katika mechi nne akipata ushindi mechi tatu na kutoa sare mechi moja huku mechi mbili kati ya tatu alizopata ushindi aliifunga Leicester City.

Hii inakuwa mara ya tatu kwa Leicester City kwenda Old Trafford msimu huu baada ya kufanya hivyo mara mbili katika mashindano ya Carabao na Ligi Kuu ambazo zote ilipoteza.

United iliingia roundi ya nne ya Kombe la FA baada ya kuiondoa Arsenal kwa mikwaju ya penati kwenye uwanja wa Emirates ambapo dakika 120 zilimalizika huku timu zote zikiwa zimetoka sare ya bao 1-1.

Kwa upande wa Leicester City yenyewe ilitinga raundi ya nne kibabe baada ya kuifunga QPR mabao 6-2 kwenye uwanja wa King Power.

Tangu alipotua Leicester City, Van Nistelrooy ameiongoza kushinda mechi mbili, sare mechi moja na kupoteza mechi nane katika michezo 11 ya mashindano yote.

Kwa United, Amorim ameiongoza kushinda mechi nane, sare mechi tatu na kupoteza mechi nane katika michezo 19 ya mashindano yote.

Beki wa Manchester United, Lisandro Martinez akiugulia maumivu baada ya kupata jeraha kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Jumapili dhidi ya Crystal Palace

United itamkosa mlinzi wa kati Lisandro Martinez ambaye alipata jeraha la mguu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Cystal Palace.

Amorim alijiunga na United Novemba mwaka jana akichukua mikoba ya Erik ten Hag huku Van Nistelrooy akijiunga na Leicester City kuchukua mikoba ya Steve Cooper ambaye alitimuliwa Novemba mwaka jana