Van Dijk awapa matumaini mashabiki Liverpool

London. Nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk amewataka mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na presha juu ya hatima yake ndani ya klabu hiyo licha ya kukiri kwamba hadi sasa hajui nini kitatokea.

Mkataba wa Dijk na Liverpool utafikia tamati mwishoni mwa msimu huu na juhudi kadhaa za uongozi wa timu hiyo kumshawishi aongeze mkataba mpya hadi sasa bado hazijafanikiwa.

Kinachotokea kwa Van Dijk pia kinafafana na mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo Mohamed Salah ambaye mkataba wake unaelekea ukingoni na hadi sasa bado hakuna dalili za kusainiwa kwa mkataba mpya.

Virgil ambaye timu yake kesho Jumapili, Machi 16, 2025 itaumana na Newcastle United katika fainali ya Kombe la Carabao, amewaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa hawatakiwi kuwa na wasiwasi kwani mambo yatakaa sawa.

“Sijui. Sijui katika hatua hii nini kitatokea lakini sitaki kutengeneza hamu ya aina yoyote au kitu kinachofanana na hicho. Naweka kichwa changu chini na kuweka mkazo wa tumaini la kushinda mechi zetu 10 zijazo.

“Huo ndio mkazo wangu wote kwa sasa. Kuwa pale kwa ajili ya meneja, wachezaji na mashabiki. Hivyo tusubirie kuona nini ambacho kitaletwa na nina uhakika mwishoni mwa msimu kutakuwa na habari. Lakini aina gani ya habari, sina uhakika,” amesema Van Dijk.

Mchezaji huyo amesema kuwa anafurahia maisha ndani ya Liverpool kutokana na hadhi ambayo imempatia katika ulimwengu wa soka.

“Kitu pekee ninachoweza kusema na nimeshakizungumza mara nyingi ni kwamba ninaona fahari kuwa nahodha wa timu hii nzuri. Hicho kina maana kubwa kwangu na kimemaanisha mengi kwangu hapo nyuma pamoja na familia yangu,” amesema Van Dijk.

Van Dijk alijiunga na Liverpool mwaka 2018 akitokea Southampton kwa ada ya Euro 84.65 milioni na tangu hapo ameichezea timu hiyo idadi ya mechi 310.

Katika mechi hizo za mashindano tofauti, Van Dijk amefunga mabao 26, amepiga pasi 13 za mwisho, akionyeshwa kadi 25 za njano na kadi moja nyekundu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *