Uyoga pori unavyogusa uchumi wa Tabora

Kwa muda mrefu Mkoa wa Tabora umekuwa ukifahamika zaidi kwa shughuli za kilimo cha tumbaku, ufugaji wa nyuki, na uzalishaji wa asali ya asili inayotamba ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, kuna sekta nyingine inayochipukia na kutoa mchango mkubwa kwa uchumi wa mkoa huu uzalishaji wa uyoga japo hauzungumzwi sana.

Katika mkoa wa Tabora, uyoga huota katika maeneo mbalimbali kama vile ardhini, kwenye vichuguu, na katika miti ya miyombo, ambayo inapatikana kwa wingi katika eneo hilo.

Uyoga ni sehemu ya kuvu inayoota juu ya ardhi na kukuza vibufu vinavyofanana na mbegu za mimea kuna uyoga unaolimwa na kuna uyoga pori.

Uyoga pori unaoliwa umegeuka kuwa fursa ya kiuchumi kwa wakazi wa Tabora, ambapo wananchi wamekuwa wakiuchuma na kuuza ili kujipatia kipato kinachowasaidia kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Thomas Charles, mmoja wa wachumaji wa uyoga wilayani Sikonge, anasema kuwa zao hilo limempa faida kubwa, kwani kwa kila msimu wa uchumaji, anaweza kupata hadi Sh20,000 kwa siku.

“Hapo awali, nilikuwa naiona biashara hii kama ndoto, lakini sasa imenibadilishia maisha,” alisema Charles.

Kwa upande wake Tatu Seif, mchumaji mwingine wa uyoga katika moja ya misitu ya Sikonge, anasema kuwa kwa sasa hana biashara nyingine zaidi ya uyoga, kwani umemletea kipato cha uhakika.

“Tuliuchukulia uyoga kama mboga ya asili tu, lakini kumbe ni fursa ya kiuchumi. Sasa ninachuma na kuwauzia watumiaji, na maisha yangu yamebadilika kwa kiasi kikubwa,” alisema Seif.

Profesa Donata Damian, ambaye ni mtaalamu wa maikrobaiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema kuwa uyoga una faida nyingi kiafya, ikiwa ni pamoja na kuongeza kinga ya mwili na hata kuimarisha nguvu za kiume.

“Uyoga siyo tu chakula cha asili, bali pia ni tiba. Unaweza kuliwa kama supu, chachandu au pilipili, hivyo ni fursa nzuri ya kiuchumi. Serikali inapaswa kuona umuhimu wa kuwekeza kwenye zao hili,” alisema Profesa Damian.

Naye mtafiti wa masuala ya misitu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Dk Numan Amanzi, anasisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa ukuaji wa uyoga.

“Kwa miaka ya hivi karibuni, uharibifu wa misitu umeongezeka, na hii imeathiri upatikanaji wa uyoga. Ili kuhakikisha zao hili linastawi, tunapaswa kulinda misitu yetu,” anasema Dk Amanzi.

Jovin Lwehabura, Mkurugenzi wa Mradi wa Maendeleo ya Maeneo Yaliyohifadhiwa (ADAP), anasema kuwa wameanzisha miradi inayowasaidia wachumaji wa uyoga kuelewa mbinu bora za uchumaji, ukaushaji, na uhifadhi wa zao hilo ili lifike sokoni likiwa katika hali bora.

“Kwa kuuchuma vizuri na kuuhifadhi ipasavyo, wafanyabiashara wa uyoga wataweza kuongeza thamani ya zao hili na kupata soko la uhakika,” alisema Lwehabura.

Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Cornel Magembe, anasema kuwa ni muhimu kwa wataalamu kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi bora ya ardhi ili kuepusha ukataji na uchomaji holela wa misitu.

“Wilaya yetu inakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira. Tunahitaji mkakati thabiti wa utunzaji wa mazingira ili uzalishaji wa uyoga uendelee kukua,” alisema Magembe.

Suzana Jeremia, mmoja wa wauzaji wa uyoga mkoani Tabora, anasema kuwa biashara hiyo imebadilisha maisha yake. “Siyo tu kwamba napata kipato kwa kuuza uyoga kwa wenyeji, lakini pia wageni wanaonunua kwa mara ya kwanza huja na marafiki zao, hivyo kuongeza wigo wa soko,” alisema Jeremia.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji mkoani Tabora, Abrahaman Mndeme, kuna njia nyingi za kuongeza thamani ya zao la uyoga.

“Uyoga unaweza kusagwa na kufungashwa kama unga katika vifungashio vya viwango mbalimbali, hali ambayo itaongeza thamani na mapato kwa wachumaji na wauzaji. Serikali iko tayari kusaidia kutoa elimu kwa wananchi ili kuimarisha biashara ya uyoga,” anasema Mndeme.

Kwa hali ilivyo, uyoga pori unaoliwa siyo tu sehemu ya utamaduni wa chakula cha asili kwa wakazi wa Tabora, bali pia ni fursa adhimu ya kiuchumi inayoweza kusaidia kuinua vipato vya wananchi na kuchangia maendeleo ya mkoa kwa jumla.

Uyoga katika soko la dunia

Kwa mwaka 2024, sekta ya uyoga duniani imeendelea kukua, ikichangiwa na ongezeko la mahitaji ya vyakula vyenye lishe bora na mbadala wa protini za wanyama. Hata hivyo, bara la Afrika linachangia kiduchu katika soko la dunia.

China ndiyo nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa uyoga, ikifuatiwa na Italia, Marekani, Uholanzi na Poland. Katika mataifa 10 vinara hakuna hata moja kutokea bara la Afrika.

Soko la uyoga unaoliwa duniani, ikiwa ni pamoja na aina zilizolimwa na za porini, lilikuwa na thamani ya dola za Kimarekani bilioni 62.55 (Sh165.44 trilioni) mwaka 2024 na linatarajiwa kufikia dola bilioni 116.26 (Sh307.5 trilioni) ifikapo 2033, likikua kwa kiwango cha asilimia 7.13.

Ingawa uyoga uliolimwa unatawala soko kwa mujibu wa kiasi na thamani, uyoga wa porini ni muhimu kwa mchakato wa kurejesha virutubisho na uchumi wa maeneo ya ndani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *