Uwepo wa Wamarekani katika kambi za kijeshi za utawala wa Israel

Gazeti la The Guardian, linalochapishwa mjini London, limeripoti kuwepo kwa maafisa wa Marekani katika mikutano ya kila siku inayofanyika katika kambi za kijeshi za utawala ghasibu wa Israel.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, maafisa wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani linalojulikana kwa jina la “USAID” wanashiriki katika mikutano ya jeshi la Israel na pia katika jela ya “Sde Teiman”, ambapo mateso ya wafungwa wa Kipalestina ni jambo la kawaida.

Kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu, baadhi ya wafungwa walioachiliwa kutoka katika gereza hilo, ambako maelfu ya Wapalestina wanazuiliwa, wanakabiliwa na dhulma na mateso makali.

Utawala habithi wa Israel kwa uungaji mkono wa Marekani ulianzisha vita vya kutisha dhidi ya Ukanda wa Gaza tangu tarehe 7 Oktoba 2023, na matokeo yake, pamoja na uharibifu mkubwa na njaa kali kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza, maelfu ya Wapalestina, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, wameuawa shahidi na kujeruhiwa.

Katika hali ya kuidhalilisha jumuiya ya kimataifa na kupuuza maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanayotaka kusimamishwa vita mara moja na kutekelezwa maagizo ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki  (ICJ)  Tel Aviv inaendelea kutekeleza mauaji ya kimbari na jinai dhidi ya wakazi wa Gaza.

Licha ya jinai zote hizo za kinyama, utawala wa Kizayuni umekiri kwamba baada ya miezi 12 ya vita bado haujaweza kufikia malengo yake ya vita hivyo ambayo ni kuiangamiza harakati ya Hamas na kuwarejesha mateka wake kutoka Ukanda wa Gaza.