
Unguja. Wakati wavuvi wadogo wakitakiwa kuachana na uvuvi haramu, kuhifadhi mazingira ya bahari, wamesema uvuaji wa kutumia tanga na mti unachangia kuathiri matumbawe chini ya bahari, hivyo kuiomba Serikali kuwapatia zana za kisasa kuimarisha uvuvi huo.
Hayo yamejiri wakati wa mafunzo ya uongozi kwa Kamati za Uvuvi ya Matemwe ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kuhusu matumizi ya rasilimali za bahari.
Akizungumza katika mafunzo hayo leo Jumatatu Aprili 21, 2025 mjumbe wa kamati hiyo, Ali Bai amesema uvuvi wa vifaa visivyo na ubora ni miongoni mwa mambo yanayochangia uharibifu na wao wapo tayari kuendesha uvuvi wa kisasa lakini changamoto kubwa ni vifaa.
“Tumepewa mafunzo, ni kweli lakini kama hakuna vifaa wavuvi wakaendela kutumia zana za kizamani inaweza kuwa kazi kubwa kufikia malengo tunayoyataka,” amesema.
Kauli hiyo imeungwa mkono na mvuvi mwingine Khamis Mcha Ali akikazia wapewe vifaa ili kunusuru kuharibu matumbawe ambayo ni maalumu kwa ajili ya mazalia ya samaki.
Ofisa Msimamizi Shirikishi wa Bahari, Maryam Ramadhan Mwinyi kutoka Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, amesema ni vyema wakaachana na uvuvi usiozingatia utunzaji wa bahari na rasimali zake kwa masilahi ya vizazi vijavyo.
Amesema kamati za uvuvi zina jukumu kubwa la kusimamia ulinzi shirikishi juu ya kupambana na uvuvi haramu usiendelee kufanyika katika maeneo ya hifadhi ili kuimarisha rasilimali zilizopo ndani yake.
“Kamati hazitakiwi kushiriki uvuvi haramu ili kuzifanya rasilimali za bahari kuwa endelevu, badala yake zinatakiwa kupambana na jambo hili kwa masilahi ya Taifa letu na kuokoa rasimali hizi zisipotee,” amesema Maryam.
Meneja Msaidizi Hifadhi ya Bahari ya Mimca, Asya Moh’d amesema iwapo kukiwa na ushirikiano itakuwa rahisi kupambana na uharibifu wa bahari lakini kila mmoja akiachiwa afanye anavyotaka inaweza ikawasumbua.
“Kamati za shehia zina mchango mkubwa katika kusimamia rasilimali za bahari, kwa hiyo lazima kushirikiana kwa pamoja kulinda na kutunza bahari yetu,” amesema.
Ofisa Uhifadhi Mazingira Baionuai na Rasilimali za Bahari, Thuwaiba Kassim Haji kutoka Idara ya Uhifadhi wa Bahari amesema Serikali imeweka utaratibu wa kufanya uchaguzi kwa kamati za uvuvi kwa lengo la kutunza mazingira ya bahari.
Amesema kuwepo kwa kamati za uvuvi kunasaidia kudhibiti uvuvi haramu usiendelee kufanyika pamoja uharibifu wa matumbawe ambao unaathiri mazalia ya samaki baharini.
Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Haji Nahoda Haji amezishauri kamati hizo kusimamia wavuvi wakati wa ukataji wa leseni kwa kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali kwa lengo la kutambua aina ya uvuvi na zana zinazotumika baharini ili kuondokana na matumizi mabaya baharini.