UVCCM yawaita vijana kujiandikisha kupiga kura, kugombea

Dar es Salaam. Katibu Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Jesca Mshama amewataka vijana kuchangamkia fursa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge katika uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 2025.

Amesema Tanzania ya sasa inahitaji viongozi vijana wenye maono mapana, weledi, uadilifu na uzalendo katika kusimamia maslahi mapana ya nchi.

Mshama, ambaye pia ni muimbaji wa nyimbo za injili kupitia kundi la J Sisters lililowahi kutamba na nyimbo kama “Rushwa” na “Tanzania” amewataka vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu kujiandisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, mzunguko wa pili, unaotarajia kuanza Mei Mosi hadi Julai 4, 2025.

Mzunguko huo wa utahusisha mikoa 31 ya Tanzania Bara, vituo 130 vya Magereza kwa Tanzania bara  na vyuo 10 vya mafunzo kutoka Zanzibar, huku jumla ya vituo 7,869 vitatumika katika zoezi hilo la uandikishaji, (ambapo Tanzania Bara kutakuwa na vituo 7,659 na Zanzibar vituo 210).

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inayonyesha mzunguko wa kwanza utaanza Mei Mosi hadi Mei 7, 2025, katika mikoa 15 ambayo ni Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe.

Mzungo wa pili utaanza Mei 16 hadi Mei 22, 2025 katika  mikoa 16, ambayo ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.

Katika taarifa hiyo, mzunguko wa tatu utaanza Juni 28 hadi Julai 4, 2025  katika vituo vya magereza (130 Tanzania Bara) na vyuo vya mafunzo (10 Zanzibar).

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumanne Aprili 30, 2025 kuhusiana uhamasisha huo, Mashama amesema mbali na vijana kujitokeza katika shughuli hiyo pia ni wakati kwa vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

“Tunaikumbusha jamii kuwa zoezi hili ni muhimu kwa kila Mtanzania kuhakikisha anapata haki yake ya msingi ya kupiga kura na kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia wa kuamua mustakabali wa nchi yetu,” amesema na kuongeza.

“Haki ya kupiga kura huanza na kujiandikisha tusikubali nafasi hii muhimu ipite bila kuchukua hatua” amesema Mshama.

Ajira kwa vijana

Katibu huyo, pia amezungumzia ukuaji wa ajira za vijana, ambapo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa awamu ya Sita kuanzia Novemba 2020 hadi Februari 2025, ajira zaidi 8,084,204, zimezalishwa, sawa na utekelezaji wa asilimia 115 ya lengo la kutengeneza ajira milioni saba katika sekta ya umma na binafsi.

“Ajira hizo zimezalishwa kupitia miradi ya kimkakati kama Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Reli ya Kisasa ya SGR, Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, pamoja na fursa za ajira katika sekta za elimu na afya” amesema.

“Pia kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri zote nchini, ambao wamewezeshwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali na kujipatia kipato halali. Takwimu zinaonesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2024 zaidi ya Sh250bilioni zimetolewa kwa vikundi vya vijana kupitia mfuko huu” alisema.

Pamoja na mambo mengine, Mshama amewataka vijana kuwa wazalendo na kulinda Amani ya nchi yao na kujiepusha na vurugu wakati wa mchakato wa kujiadikisha na kuborsha taarifa zao na badala yake .

“UVCCM tunawataka vijana wote wa Kitanzania kuchangamkia fursa hizi, kuwa wazalendo kwa taifa lao, na kamwe wasikubali kutumika vibaya na watu wasiolitakia mema taifa letu. Ushiriki wetu wa sasa ndio unaojenga Tanzania ya kesho yenye nguvu, haki, maendeleo na amani ya kudumu” ameongeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *