
Waandishi wa habari kumi wa Uturuki, akiwemo mpiga picha kutoka shirika la habari la AFP, wamekamatwa siku ya Jumatatu, Machi 24, nyumbani kwao huko Istanbul na Izmir (magharibi), jiji la tatu kwa ukubwa nchini humo, shirika la haki za binadamu la Uturuki MLSA limeripoti.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Kukamatwa huku kulifanyika siku moja baada ya maandamano mapya yaliyochochewa na kukamatwa kwa meya wa upinzani, pia akiwa kiongozi wa upinzani wa Istanbul Ekrem İmamoğlu, ambaye anazuiliwa jela tangu siku ya Jumapili Machi 23, 2025.
Polisi wamewakamata waandishi wa habari tisa katika msako wa mapema asubuhi katika miji kadhaa, ukiwalenga wale ambao walikuwa wameripoti maandamano kufuatia kukamatwa kwa Meya wa Istanbul Ekrem İmamoğlu. Aidha, mwandishi wa habari aliwekwa chini ya ulinzi katika eneo la maandamano jana usiku.
Kukamatwa kwa watu hao kunakuja wakati maandamano yakiendelea kote nchini, ikiwa ni pamoja na katika uwanja wa Saraçhane wa Istanbul, karibu na jengo la Manispaa ya mji huo.
Wapigapicha wawaliokuwa wakipiga picha vitendo vya polisi wakati wa maandamano hayo ni miongoni mwa waliokamatwa. Mamlaka haijasema mashtaka dhidi yao.
Tangu maandamano hayo yaanze Machi 19, waandishi wa habari kadhaa wamejeruhiwa wakati wa uingiliaji kati wa polisi walipokuwa wakiripoti matukio katika maeneo ya matukio. Polisi pia wameripotiwa kuharibu vifaa vya waandishi wa habari katika visa vingine. Matukio haya yamelaaniwa na vyama vya wanahabari.
“Usalama wa waandishi wa habari unatishiwa”
Mashirika yanayotetea uhuru wa habari na miungano ya waandishi wa habari imelaani kukamatwa kwa watu hao. Erol Önderoğlu, mwakilishi wa shirika la Wanahabari Wasio na Mipaka (RSF) nchini Uturuki, amesema: “Mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari hayaonyeshi dalili za kupungua. Usalama na haki za wanahabari zinakiukwa. Tunatoa wito kwa Waziri wa Mambo ya Ndani kukomesha ukiukwaji huu.”
Chama cha Wanahabari nchini Uturuki (TGS) kimesema: “Waandishi wa habari wanaotekeleza wajibu wao wa kuhabarisha wanalengwa. Achani sera yenu ya shinikizo na udhibiti dhidi ya waandishi wa habari.”
Umoja wa Wanahabari wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Wanaoendelea (DİSK Basın-İş) umesema: “Kukamatwa kwa waandishi wa habari wakati wa msako nyumbani kwao kunajumuisha shambulio la uhuru wa waandishi wa habari na haki ya umma ya kupata habari. Kuwanyamazisha waandishi wa habari hakutaficha ukweli.”