
Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK) kimetangaza kuvunjwa kwake rasmi Jumatatu, Mei 12, na kumaliza zaidi ya miongo minne ya mapambano ya kijeshi dhidi ya taifa la Uturuki, shirika la habari linalounga mkono Wakurdi ANF limeripoti. Mnamo Mei 9, PKK ilitangaza kuwa imefanya kongamano lake, kwa nia ya kuvunjwa kwake, “kwa mafanikio.”
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
“Bunge la 12 la PKK limeamua kuvunja muundo wa chama cha PKK na kukomesha mbinu ya mapambano ya kijeshi,” kundi la Wakurdi lenye silaha limetangaza katika taarifa yake, baada ya awali kueleza kuwa lilifanya mkutano wake wiki iliyopita.
Mnamo Februari 27, kiongozi wa kihistoria wa PKK, Abdullah Öcalan, alitoa wito kwa vuguvugu lake kuweka chini silaha na kumaliza vita vya msituni ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 40,000 tangu mwaka 1984. Wito huu wa Abdullah Öcalan, anayefungwa kwa miaka 26 katika kisiwa cha gereza cha Imrali, karibu na mwambao wa Istanbul, umefuatia upatanishi ulioanzishwa msimu wa vuli na mshirika mkuu wa rais Recep Tayyip Erdoğan, Devlet Bahçeli, kupitia chama kinachounga mkono Wakurdi DEM.
Kundi la PKK lilijibu vyema mnamo Machi 1 wito wa kiongozi wake wa kihistoria, na kutangaza kusitisha mapigano mara moja na vikosi vya Uturuki. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan alisema wakati huo wito wa Abdullah Öcalan ulikuwa “fursa ya kihistoria” kwa Waturuki na Wakurdi, ambao wanawakilisha, kwa makadirio fulani, 20% ya wakaazi milioni 85 wa Uturuki.